Na Allan Kitwe, Tabora
WATUMISHI wa Halmashauri ya Manispaa Tabora wametakiwa kutekeleza wajibu wao kwa weledi na uadilifu mkubwa ili wananchi wafurahie matunda ya nchi yao na waendelee kuiamini serikali yao ya Chama Cha Mapinduzi.
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tabora Mjini Mohamed Katete alipokuwa akitoa salamu za chama kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kilichofanyika leo katika ukumbi wa manispaa.
Amesema kuwa chama kinaridhishwa na kasi ya utekelezaji miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo katika sekta zote kwani hata kero za upatikanaji huduma mbalimbali zimepungua sana katika manispaa hiyo.
Amebainisha kuwa serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imeleta fedha nyingi sana katika halmashauri hiyo ili kutekeleza miradi mbalimbali na matunda ya miradi hiyo sasa yanayonekana.‘Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuleta fedha nyingi za miradi ya maendeleo, rai yangu kwa watumishi wote wa manispaa ni kufanya kazi kwa bidii na weledi mkubwa na kuwa waadilifu ili wananchi wanufaike’, amesema.
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1001654408-1024x768.jpg)
Katete amedokeza kuwa baadhi ya watumishi wamekuwa wakitanguliza maslahi binafsi kwenye miradi ya maendeleo hali inayofanya miradi hiyo kuchelewa kukamilika au kutekelezwa chini ya kiwango, hilo halikubaliki.
Amempongeza Mstahiki Meya, Mkurugenzi Mtendaji, Mkuu wa Wilaya na Waheshimiwa madiwani kwa kusimamia vizuri mabilioni ya fedha yanayoletwa na serikali kwa ajili ya utekelezaji miradi ya wananchi.
‘Wataalamu mnafanya kazi nzuri, lakini baadhi yenu sio waadilifu, ninyi ndio mnaorudisha nyuma juhudi za Mheshimiwa Rais za kuwaletea maendeleo wananchi, badilikeni, la sivyo hatua zichukuliwe,’ ameonya.
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/mkoa3-1024x768.jpeg)
Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Tabora Daniel Mhina amepongeza ushirikiano mzuri wa Ofisi ya Mkurugenzi na Watumishi wake hali inayofanya yeyote anayeachiwa Ofisi hiyo kufanya kazi kwa weledi mkubwa.Ameshauri Ofisi ya Mkurugenzi kutofumbia macho watumishi wanaoenda kinyume na maadili ya kazi zao na hatua zichukuliwe ili wananchi waendelee kufurahie huduma bora zinazotolewa na halmashauri yao.Aidha amewataka kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ili kuharakisha utekelezaji miradi ya maendeleo na kuboresha utoaji huduma kwa jamii katika maeneo yote.
More Stories
Wasira ‘aipiga nyundo ‘No reform no election
Tabora wapongeza uimara wa CCM
CCM yahimiza uadilifu kwa watumishi Manispaa Tabora