December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM yahamasisha usajili wanachama kidigitali

Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM),mkoani Mwanza,katika kuongeza idadi ya wanachama kimewahimiza wana CCM wakiwemo wananchi kujitokeza kuchukua kadi mpya za kielektroniki na kusajiliwa katika mfumo huo kwa kuchangia gharama ya sh.2,000.


Rai hiyo imetolewa kwa nyakati tofauti na Katibu wa Itikadi,Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa Mwanza,Prudence Sempa, wakati akizungumza na wajumbe wa kamati za siasa za Kata za Buzilasoga wilayani Sengerema na Mhande katika Wilaya ya Kwimba.

Amesema baada ya uchaguzi mdogo wa Udiwani katika Kata za Buzilasoga na Mhande kumalizika,wanaCCM wahakikishe wanawahimizwa kuchukua kadi za kielektroniki kwa sh.2,000 na kusajiliwa katika mfumo huo wa kisasa.

Pia amesema baada ya uchaguzi mdogo wa udiwani kumalizika, watu wahamasishwe wakajiandikishe katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,wapate fursa ya kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu lakini pia wasio na vyama na wanachama wa vyama vingine vya siasa wajiunge na CCM.

Sempa amesema kadi hizo za kisasa za CCM zina faida nyingi kulinganisha na za vyama vingine, kutokana na kuunganishwa na mifumo ya huduma za matibabu,NIDA, fedha,hati za usafiri na huduma zingine.

Kwa mujibu wa Katibu Mwenezi huyo tayari Mkoa wa Mwanza umepokea kadi za kielektroniki 79,986 na kuwataka makatibu wa wilaya kuchangamkia fursa hiyo huku akiwaasa wahakikishe fedha za mauzo ya kadi hizo zinawasilishwa makao makuu zichapwe zingine.

Amewataka wananchi na wana CCM kuchapa kazi ili kuwaunga mkono viongozi wa Serikali na chama na kuwatia moyo wa kuendelea kuwahudumia na kuwatumikia kwa ajili ya maendeleo ikizingatiwa kazi ni kipimo cha utu.

Aidha amewahamasisha wananchi wakiwemo wana CCM kujitokeza kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu kwa kuchagua viongozi wa kuwatumikia kama ilivyo kauli mbiu ya Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Uadilifu Kazi Iendelee.