Na Esther Macha,TimesMajiraOnline,Mbeya
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kupitia ilani yake ya mwaka 2025/2030 kimeahidi kuendelea kutoa mbolea za ruzuku, viwatilifu na pembejeo nyingine za kilimo ili kuongeza tija kwa wakulima.
Ahadi hiyo imetolewa Septemba 30, 2025 na Mgombea Ubunge wa Jimbo la Uyole, Dkt. Tulia Ackson, wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Iganjo ikiwa sehemu ya ziara yake ya kunadi ilani ya chama.
Kilimo cha kisasa
Dkt.Tulia amesema serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuhakikisha kilimo kinakuwa cha kisasa na chenye faida kwa wakulima.
“Ruzuku maana yake ni kuwa wananchi wananunua pembejeo kwa bei nafuu.
Ilani ya CCM ya 2025/2030 inasisitiza mpango huu na tayari mbolea za ruzuku zimeongezeka. Wananchi wa Iganjo wote tutafikiwa, changamoto za msimu uliopita zinaenda kuisha kwa sababu tumepata uzoefu,”amesema.
Aidha, amebainisha kuwa skimu za umwagiliaji zilizopo katika Kata ya Iganjo zitaendelea kuboreshwa kupitia utekelezaji wa ilani hiyo.
Sekta ya Nishati
Akizungumzia sekta ya nishati, Dkt.Tulia amesema ilani ya CCM 2025/2030 imeweka mkazo kwenye upatikanaji wa umeme vijijini na maeneo yote ambayo bado hayajafikiwa.
“Kwa sasa tayari utekelezaji umeanza Hapa Iganjo tutajengewa kituo kikubwa cha umeme ili kukabiliana na changamoto za kukatika kwa umeme na kusuasua kwa upatikanaji wake. Hii ndiyo maana halisi ya miaka mingine mitano ya Rais Samia – kuendeleza kazi kubwa aliyoianza,” amesema .
Wito wa kuamini CCM
Kwa upande wake, Diwani Mteule wa CCM Kata ya Iganjo, Eliud Mbogella, amewataka wananchi kuendelea kuiamini CCM kwa sababu ya maendeleo yanayoonekana katika nyanja za afya, elimu na maji.
“Wananchi wa Iganjo tumepata manufaa mengi kupitia Mbunge wetu Dkt. Tulia hata akiwa Mbunge wa Mbeya Mjini. Sasa amekuja nyumbani, naamini tutapata maendeleo makubwa na changamoto nyingi zitamalizika,”amesema.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi