December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM Mwanza yaanika mafanikio ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi

Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza kimesema kimefurahishwa na utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ambapo miradi ya maendeleo yenye zaidi ya bilioni 200 imetekelezwa kwa weledi na kupongeza mradi wa maji Kagunguli-Bukindo kuokoa kiasi cha milioni 326 kati ya bilioni 2.5 za mradi.


Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Michael Masanja ‘Smart’ akifungua mkutano wa Halmashauri Kuu ya chama hicho ambapo ameeleza kuwa miradi walioikagua iko vizuri,hivyo maelekezo walioyatoa wakati wa ukaguzi yazingatiwe ili ikamilike kwa wakati.

Smart amesema uchumi mkubwa wa Mwanza unategemea zao la pamba ambalo uzalishaji wake unashuka kila uchao,hivyo serikali ione namna ya kusimamia na kuboresha kilimo cha zao hilo pia uvuvi usimamiwe vyema kwa kudhibiti uvuvi haramu samaki waongezeke watu wafanye biashara.

“Mkuu wa Mkoa ukiendelea hivi NCU (Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza) itafanya kazi vizuri chini yako.Pia, mwaka huu ni wa uchaguzi wa serikali za mitaa,tuisemee miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na serikali,”.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda,akiwasilisha utekelezaji wa ilani ya CCM 2020-2025,amesema miradi ya maendeleo ya wananchi ya sh. bilioni 212.7 imetekelezwa mkoani humo ndani ya miaka mitatu.

Amesema miradi hiyo ni ya sekta ya elimu,maji,afya,michezo na miundombinu ya barabara ikiwemo vyombo vya usafiri wa majini.