January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM kusomesha udereva wasichana 36

Na Agnes Alcardo,TimesmajiraOnline,Dar

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Mbeya kimeahidi kuwalipia ada ya mafunzo ya udereva vijana wa kike 36, kutoka Kata zote za Mbeya Jiji, ambapo kila Kata atachukuliwa msichana mmoja.

Ahadi hiyo imetolewa Septemba 21, 2024 na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Patrick Mwalunenge, kwenye Kongamano la mabinti lililofanyika Jijini humo, akiwasihi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la makazi litakaloanza Octoba 11 mwaka huu, kushiriki kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

“CCM kupitia Mimi mwenyewe Mwenyekiti katika Mkoa huu,tutawalipia ada ya kujifunza udereva mabinti 36 kutoka Kata zote za Mbeya Jiji, kwa maana hiyo kila Kata itatoka binti mmoja na jambo hili litakuwa ni muendelezo tulimaliza hao tutachukua wengine, lakini suala la muhimu kwa kipindi hiki ni Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hivyo niwaombe mjitokeze kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la makazi tayari kwa ajili ya kushiriki uchaguzi lakini pia kwa wenye sifa kugombea nafasi za uongozi”,amesema Mwalunenge.

Aidha,amewataka vijana hao wa kike kujitengenezea mfumo wa kujiwekea pesa kupitia vikundi ili waweze kujikwamua kiuchumi,kwani kupitia vikundi hivyo kutawasaidia kukopa pindi wanapokuwa na uhitaji,ambapo tayari chama kupitia Mwenyekiti huyo kimetoa Sh. Mil 1 kwa ajili ya kusaidia kutunisha mfuko wao.

Sambamba na hayo, amewataka vijana hao kunitumia vizuri mitandao ya kijamii ili iwaingizie kipato ” Ni vyema mkatumia vizuri mitandao ya kijamii ili muweze kujiingizia kipato na si vinginevyo, unakuta mtu anapiga selfie alafu anaposti Instagram hiyo inakusaidia nini? badala ya kufanya kitu Cha maana na ukakiposti kikakuletea manufaa”, ameongeza.

Hata hivyo, ameendelea kuwasisitizia vijana hao wa kike kutokubali kutumika vibaya na baadhi ya watu wenye nia hovu hususani wanasiasa, ambao wamekuwa wakileta uchochezi kupitia mitandao ya kijamii, akisema kuwa kufanya hivyo ni uvunjifu wa amani.