January 27, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM ilivyotambua mchango wa wanahabari Mkutano Mkuu Maalum

Na Agnes Alcardo

WAKATI dunia ikiendelea kukipongeza Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kufanya Mkutano Mkuu Maalum wa kihistoria Januari 18-19, 2025 , Dodoma, chama hicho kimeweka historia ya kuwaheshimisha Wanahabari.

Katika mkutano huo, CCM kiliweka historia ya kualika idadi kubwa ya Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali Tanzania Bara pamoja na visiwani Zanzibar.

Pia chama hicho kiliwaalika wanahabari wakongwe wakiwemo wastaafu na wale ambao bado wanaendelea na kazi ya uandishi katika baadhi ya vyombo vya habari.

Baadhi ya wanahabari hao ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ithibati ya Habari, Tido Mhando na Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura.

Wengine ni Mhariri Mtendaji wa zamami TSN, Charles Rajabu, Halima Kihemba, Salva Rweyemamu, Ahmed Kipozi, gwiji wa utangazaji Theophil Makunga na Angetile Osiah.

Waandishi wengine wakongwe ni John Bwire, Absalom Kibanda, Jesse Kwayu, Bakari Machumu, Saed Kubenea, Mbaraka Islam, Pascal Mayalla, Antal Sangali, Dkt. Ayoub Rioba na wengine mengi.

Kwa hakika, Sekretarieti ya CCM Taifa imefanya jambo kubwa la heshima kuwaalika wanahabari kutoka vyombo vyote nchini pamoja na mitandao ya kijamii, ikiwa ni tofauti na mikutano mikuu mingine, kwani mkutano huo vyombo vya Habari vilishirikishwa kwa asilimia 100.

Ushiriki mkubwa wa wanahabari katika Mkutano huo, umelifanya tukio hilo kuwa la kimataifa, siku mbili za mkutano huo, dunia nzima imejua CCM ilikuwa na tukio gani la kihistoria likionekana na kusikika ‘Mubashara’ kupitia mitandao ya kijamii, redio na televisheni na magazeti.

Pongezi kubwa ziwaendee wanahabari wakongwe ambao kwa sasa wapo Makao Makuu ya CCM ambao ni Dennis Msacky ambaye ni Msaidizi wa Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi.

Mwingine ni Aboubakary Liongo ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mawasiliano katika Idara ya Uenezi, Itikadi na Mafunzo Makao Makuu ya CCM Taifa.

Wanahabari hao waliwelewa mazingira mazuri yaliyokuwa rafiki kwao katika ufanyaji wa kazi zao, ikiwa pamoja na “Screen” kubwa zilizokuwa zimewekwa kwenye eneo lao ili kuweza kufuatilia matukio ya mkutano yaliyokuwa yakiendelea kipindi wawapo nje.

Kwa kutambua umuhimu wa mkutano huo, Wanahabari hao walifanya kazi kubwa ya kuhakikisha, dunia inajionea na kusoma matukio yote katika kikao hicho ‘Mubashara’ kupitia vyombo mbalimbali vya habari.

Kupitia vyombo vya habari na wanahabari walioalikwa katika mkutano huo, Watanzania na dunia nzima walipata fursa ya kujionea jinsi chama tawala CCM kilivyoweza kuwasilisha ajenda zake kwa wajumbe.

Mkutano huo uliongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ukiwa na ajenda kuu tatu.

Ajenda hizo ni kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara; kupokea taarifa ya kazi za chama kuanzia 2022-2025; kupokea taarifa ya utekelezaji Ilani ya Uchaguzi ya CCM.  

Mbali ya ajenda hizo, wajumbe waliibua hoja za mkutano huo kupitisha azimio la kumteua Rais Dkt. Samia kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuwa mgombea urais Zanzibar.

Mkutano Mkuu Maalum wa CCM ndiyo chombo cha mwisho cha maamuzi ya uteuzi wa mgombea urais kwa tiketi ya urais kupitia chama hicho, pia mkutano huo ulipitisha jina la mwanasiasa mkongwe na kada wa CCM Stephen Wassira kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara akichukua nafasi ya Abdulrahman Kinana aliyeomba kupumzika.

Vyombo vya habari ni mhimili wa nne wa dola vikiwa daraja kati ya wananchi na mihimili mingine.

Serikali inayoongozwa na CCM imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuhakikisha vyombo hivyo vinafanya kazi yeke kwa ufanisi, maendeleo ya wananchi na Taifa.

Vyombo hivyo vinafanya kazi kubwa ya kuhabarisha, kuelimisha, kuburudisha na kuchochea mijadala ambayo imekuwa na matokeo chanya kwa maendeleo ya nchi.
Huwezi kusungumzia maendeleo ya Taifa lolote duniani bila kuvitaja vyombo vya habari ambavyo ni televisheni, magazeti, redio, mitandao ya kijamii vikiwa na nguvu kuiunganisha jamii na serikali inayowaongoza.

KUONGEZA UFAHAMU

Vyombo vya habari vina jukumu la kutoa taarifa muhimu kwa umma kuhusu matukio yanayotokea ndani na nje ya nchi, Kupitia habari, watu wanaweza kufahamu masuala ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.

Ufahamu huo unawasaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi kuhusu maisha yao binafsi na masuala ya kijamii.

KUIMARISHA DEMOKRASIA

Vyombo vya habari vina mchango mkubwa wa kuimarisha demokrasia kwa kutoa jukwaa la mijadala, taarifa ambazo zinawasaidia wananchi kufanya maamuzi yenye uelewa zaidi.

Pia vyombo vya habari hutoa taarifa kuhusu shughuli za serikali, uchaguzi na masuala ya kisiasa hivyo kuwapa wananchi nafasi ya kuhoji viongozi na kushiriki kikamilifu katika demokrasia.

UWAJIBIKAJI WA VIONGOZI

Kupitia uchunguzi na utoaji wa taarifa za kina, vyombo vya habari vina uwezo wa kufuatilia na kuripoti kuhusu uwajibikaji wa viongozi wa serikali, taasisi za umma.

Kwa kufichua ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka, vyombo vya habari vinawashinikiza viongozi kuwajibika kwa wananchi, kuchukua hatua dhidi ya ufisadi.

KUUNGANISHA JAMII

Vyombo vya habari vinatoa taarifa zinazounganisha watu wa jamii moja, Mkoa mmoja, nchi nzima, kupitia taarifa za habari, watu wanajua masuala yanayoathiri jamii nzima, kushirikiana kutafuta suluhisho.

Kwa mfano, habari za maafa au matukio ya kitaifa huwaleta watu pamoja, kusaidiana na kuonyesha mshikamano.

KUBURUDISHA

Mbali na kutoa habari, vyombo vya habari vinatoa burudani kwa njia ya michezo, muziki, filamu, vipindi vya ucheshi.

Burudani ni muhimu kwa afya ya akili, kusaidia watu kupumzika baada ya kazi na shughuli za kila siku. Pia ni njia ya kuhamasisha vipaji na kukuza sekta ya sanaa.

KUELIMISHA

Vyombo vya habari vina jukumu kubwa la kuelimisha jamii kuhusu masuala mbalimbali kama afya, kilimo, biashara na maendeleo ya teknolojia.

Kupitia vipindi maalum vya elimu, wananchi hujifunza mambo mapya ambayo yataboresha maisha yao, kupata maarifa ya kukabiliana na changamoto za maisha. Elimu hiyo inasaidia kuongeza tija, ufanisi katika jamii.

KUKUZA UCHUMI

Vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika ukujai wa uchumi kwa njia mbalimbali ikiwemo ya kutangaza biashara, bidhaa pamoja na huduma.

Matangazo hayo huleta wateja kwa wafanyabiashara hivyo kusaidia kuongeza mapato. Pia vyombo vya habari vinaajiri watu wengi hivyo kupunguza tatizo la ajira.

KUHAMASISHA

Pia vyombo vya habari vina nafasi ya kuhamasisha mabadiliko chanya katika jamii kwa kuhamasisha umma kuchukua hatua.

Kupitia uandishi wa habari, vyombo vya habari vinaweza kuibua changamoto za kijamii kama unyanyasaji kijinsia, umaskini, unyanyapaa hivyo kuhamasisha juhudi za kuboresha hali hizo.

KUENDELEZA UTAMADUNI

Vyombo vya habari vinasaidia kuhifadhi na kueneza utamaduni wa jamii mbalimbali kwa kutoa vipindi na maudhui yanayoelezea mila, desturi za jamii hizo.

Hatua hiyo inasaidia kuwaunganisha watu na urithi wao wa kiutamaduni, kuongeza fahari ya kitaifa. Pia vyombo vya habari husaidia kukabiliana na changamoto za athari za utandawazi kwa kuhifadhi utambulisho wa jamii.

MABADILIKO KISIASA

Vyombo vya habari vina nguvu ya kuleta mabadiliko ya kisiasa na kijamii kwa kufichua udhaifu wa sera au matatizo yanayohitaji kutatuliwa.

Kwa kuripoti kuhusu masuala ya kijamii, kutoa jukwaa la mijadala, vyombo hivyo vinaweza kusaidia kufanikisha mabadiliko muhimu katika sera za kitaifa, kushawishi wanasiasa kuchukua hatua.

SAUTI YA WATU

Vyombo vya habari hutoa jukwaa ambalo watu wa rika, makundi tofauti wanaweza kueleza hisia zao, mawazo, maoni yao hasa wenye uwezo mdogo wa kufika kwenye vyombo vya maamuzi, hutoa sauti zao kupitia vyombo vya habari, kueleza changamoto walizonazo.

Vyombo vya habari vina umuhimu mkubwa katika jamii kwa kuwa ni daraja kati ya serikali, wananchi vikichochea demokrasia, kuimarisha uwajibikaji, kuboresha maisha ya watu, kuelimisha na kuburudisha.

4R ZA RAIS SAMIA

Matokeo ya mageuzi ambayo Rais Dkt. Samia anaendelea kuyasimamia kupitia 4R zake, yanazidi kuonekana kupitia sekta mbalimbali ambapo utashi wake kisiasa umeendelea kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari.

Tangu aingie madarakani Machi 19, 2021, uongozi wa Rais Dkt. Samia umekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha uhuru, hali ya kiuchumi ya vyombo hivyo.

Uthibitisho huo umeonekana kwenye ripoti ya ‘Reporters Without Boarders (RWB) iliyoitaja Tanzania kuwa namba moja Afrika Mashariki kwa kulinda uhuru wa vyombo vya habari.

Utafiti huo umeonesha kuwa, Tanzania imepiga hatua kubwa duniani ikipanda kutoka nafasi ya 143 mwaka 2023 hadi nafasi ya 97 mwaka 2024.

Pia utafiti huo uliangazia mambo mbalimbali yakiwemo misingi ya kisheria, hali ya kiuchumi, kisiasa, usalama wa wanahabari, dhana ya kijamii na kitamaduni.

Hayo ni matokeo ya dhamira ya Rais Dkt. Samia kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari kwani alipoingia madarakani, aliyafungulia magazeti na televisheni za mitandaoni ambazo zilikuwa zimefungiwa.

Ameunda kamati iliyokamilisha kazi ya kuangalia hali ya kiuchumi kwa vyombo vya habari na kuruhusu taasisi za serikali kupeleka matangazo katika vyombo vya habari.

Madanikio hayo yamechangiwa na mabadiliko ya Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari Mwaka 2026, baadhi ya Kanuni za Sheria ya Mawasiliano ya Kielekroniki na Posta (EPOCA) 2010.

Pia mikakati wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kutoa elimu ya sheria za utangazaji na kimtandao hivyo kuviwezesha vyombo vya habari kuzingatia sheria.
Mwaka 2022, Rais Dkt. Samia aliweka rekodi ya kuwa Rais wa Kwanza kushiriki maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari, jijini Arusha.

Hatua hiyo ilidhihirisha dhamira yake ya kukuza sekta hiyo ambayo imetoa ajira kwa maelfu ya vijana, kuonesha namna inavyotambua mchango wa vyombo vya habari katika maendeleo ya Tanzania.

Kupitia makala hii, nashawishika kusema CCM imeweka historia ya kuwatambua, kuwathamini wanahabari kwa kuwapa nafasi ya kushiriki Mkutabo Mkuu Maalum uliofanyika jijini Dodoma, Januari 18-19, 2025.