November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM Bagamoyo yaridhishwa utendaji wa Rais Samia

Na Mwnadishi Wetu,TimesmajiraOnline,Bagamoyo

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, kimetoa tamko la kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Rais Samia Suluhu.

Tamko hilo limetolewa mbele ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, iliyokuwa chini ya Mwenyekiti wake, Alhaj Abdul Sharifu, katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete.

Tamko hilo lililosomwa na Katibu Mwenezi, Ramadhani Lulanga, limeeleza kuwa wana CCM Bagammoyo wanaridhishwa na kazi inayoendelea kutekelezwa na Rais Samia, katika nyanja mbalimbali.

“Pamoja na kukabiliwa na majukumu ya Kitaifa, lakini Mwenyekiti wetu anaendelea kuwatumikia Watanzania katika myanja mbalimbali, wana CCM Bagamoyo tunampongeza kwa kazi iliyotukuka,” ilisema

“Katika kipindi cha miaka mitatu ya utawala wake, ametumia nafasi hiyo vizuri ya kuitangaza nchi, kwetu wana Bagamoyo tunapokea wawekeaji kila kukicha wanaotokea nchi mbalimbali,” ilieleza taarifa hiyo.

“Sanjali na hayo amemalizia daraja la Wami, ujio wa Bandari ya Bagamoyo ikiwemo kituo cha kupoozea umeme kinachojengwa Kitongoji cha Pera hapa Chalinze,” ilimalizia taarifa hiyo.

Awali Sharifu aliwaambia wajumbe hao kwamba miaka mitatu ya Rais Samia ameonesha kuwa ni Mama mwenye uwezo wa kuongoza na kwamba dhana na dhima ya kusema akimama wakiwezeshwa wanaweza ni ya kweli.

“Kwa niaba ya wana Bagamoyo tunapongeza, kwani kazi kubwa anaifanya ndani ya wilaya yetu, miradi mingi ya maendeleo imeletwa, kwa kweli Mama amefanyakazi kubwa tumpe pongezi nyingi sana”, alisema Sharifu.

“Upande wa uchaguzi hakuna goli la penati, Rais Samia amesema mgombea anayepita pasipokupingwa naye apigiwe kura ya ndio au hapana,” alisema Mwenyekiti huyo.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalumu mkoani Pwani, Subira Mgalu aliwaambia wajumbe hao kuwa (UWT) wamemshukuru Rais na kwamba wamepitisha sheria tatu bungeni ambazo Machi 25 Rais amesaini.

Sheria hizo ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani, Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi na Sheria ya Vyama vya Siasa, upande wa uchaguzi ya Rais Wabunge na Madiwani limeongezwa kosa la ukatiri wa kijinsia kuwa miongoni mwa makosa ya uchaguzi,” alisema Mgalu.

Aliongeza kwamba katika uchaguzi wa wenyeviti wa vijiji na vitongoji utasimamiwa na Tume ya Uchaguzi.

“Rai yangu tusidharau bora tutoke jasho jingi wakati huu wa neema ya utulivu, lakini ikija Iyena iyena tuwe tumeishamaliza kazi,” alisema.