November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCK wazindua sera ya kijinsia

Na Mwandishi wetu, Timesmajira online

CHAMA Cha Kijamii (CCK) kimezindua sera ya kijinsia yenye lengo la kuwawezesha wanawake ndani ya Chama hicho kushiriki katika ngazi mbalimbali za maamuzi.

Akizungumza katika hafla hiyo ya Uzinduzi iliyofanyika Jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera,Bunge na Uratibu Jenista Mhagama,Mwenyekiti wa Taifa Chama Cha UPDP, Twalib Kadege amesema kuwa sera hiyo inahimiza uongozi unaozingatia usawa wa kijinsia ambao unaleta maendeleo chanya katika jamii .

“Kupitia sera hii ya kijinsia itasaidia kuleta usawa kwa Taifa katika kuwapata viongozi wenye kuleta tija kwa Taifa kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mtaa unatarajia kufanyika mwaka 2024 pamoja na uchaguzi mkuu mwaka 2025″amesema

Na kuongeza kuwa
“Sera hii itasaidia kuwaamsha wenye uhitaji maalum kushiriki kwa wingi sawa na wanaume kwenye harakati za kisiasa kwa kuona sasa kuna sera inayowalinda na wao kupata nafasi kubwa za kiuongozi”aliongeza

Awali mwenyekiti wa Chama Cha Kijamii (CCK) David Mwaijojele, amesema kuwa sera ya kijinsia italeta ahueni katika kuhakikisha changamoto mbalimbali zinapatiwa majibu kupitia mikakati ambayo inampa fursa mwanamke kugombea na kupata nafasi katika ngazi mbalimbali.

“Mchakato huu wa uandishi wa sera ya Kijinsia ulifanyika septemba 2022 kufuatia ofisi ya msajili wa vyama vya siasa na baraza la vyama vya siasa sambamba na mashirika mbalimbali yakiwemo la
MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP), Chama cha Wanawake katika sheria(WILDAF), Umoja wa Wanawake Wanasiasa, (ULINGO) kukaa na kuunga mkono suala la vyama vya siasa kuunda sera ya ushiriki wa wanawake na makundi maalumu”amesema

Amesema kuzinduliwa kwa sera hiyo ni matunda ya muda mrefu kutokana na kuwepo kwa mjadala kuhusu wanawake na makundi maalum kushiriki katika nafasi mbalimbali .

“Tumeizindua sera hii itatumika katika ngazi ya chama chetu na kuwapiga chapuo wanawake kupata nafasi katika suala la uongozi’amesema Mwenyekiti Mwaijolele

Naye Mwenyekiti wa Bodi Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Gemma Akilimali, amesema kuwa wanawake wanauwezo wa kufanya mambo makubwa kama wakipewa nafasi katika uongozi, hivyo sera hiyo itakuwa ni rafiki katika kufikia malengo.

Aliupongeza uongozi wa CCK kwa hatua hiyo ya kizindua sera za jinsia kukubalika katika vyama vya siasa kwani wamefanyia kazi kwa muda mrefu katika kujenga usawa kwenye nyanja mbalimbali.

“Suala la jinsia ni mahusiano katika jamii ambayo yanadai kuwa na usawa katika nyanja mbalimbali ikiwemo uongozi au hata katika kumiliki rasilimali lakini tunachukua kiini cha uongozi’amesema Akilimali

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji WILDAF Anna Kulaya amewataka wanachama wa CCK kuisoma sera hiyo na kuielewa ili wafahamu wanawajibu gani wa kuitekeleza kwa ufasaha

Aidha alitoa wito kwa Vyama vya Siasa Nchini kuinga mfano wa Chama Cha CCK Kwa kuwa na sera ya Jinsia katika vyama vyao ili kuhakikisha vyama vinafanya michakato yake ya ndani na kuandaa viongozi wa kitaifa kulingana na usawa wa jinsia

uzinduzi wa sera ya kijinsia ulienda sambamba na uchaguzi Mkuu wa chama hicho.

Mwenyekiti Taifa wa Chama Cha UNDP, Twalib Kadege akizungumza katika hafla hiyo ya Uzinduzi wa sera.
Baadhi ya wanachama wa Chama Cha kijamii CCK walioudhulia katika hafla hiyo ya Uzinduzi sera hiyo.
Mwenyekiti wa bodi TGNP, Gemma Akilimali akizungumza katika hafla hiyo