Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
HOSPITALI ya CCBRT kwa kushirikiana na Light for the World imeanzisha kampeni ya upimaji wa macho kwa watoto chini ya miaka tano lengo likiwa kupunguza matatizo ya macho kwa watoto hapa nchini.
Akizungumza katika zoezi la utoaji wa matibabu hayo katika Zahanati ya Mbande iliyopo wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, Dkt.Picard Adubango alisema lengo kuwa la kampeni hiyo ni kuhakikisha watoto chini ya miaka mitano wanapimwa macho na kupatiwa matibabu bure.
“Lengo ni kupunguza kiwango cha wagonjwa wa macho nchini, ndiyo maana tumeanza kampeni hii kwa watoto chini ya miaka kwani ni rahisi kubaini ugonjwa uliopo na kumpatia matibabu katika umri huo na itaondoa tatizo la maradhi ya macho kwake kwa miaka ya baadae,” alisema Dkt.Adubango.
Alisema tatizo la macho limekuwa kubwa hapa nchini hii imetokana na kutofanya uchunguzi hasa kwa watoto hali inayopelekea ugonjwa kukua kadri ya miaka inavyoongezeka, hivyo kwa kufanya uchunguzi wa mara kwa mara utasaidia kupunguza tatizo la macho nchini Tanzania.
“Tumeanza katika zahanati ya Mbande na tutaendelea na kampeni hii katika zahanati nyingine katika maeneo mbalimbali nchini lengo likiwa ni kuwafikia watoto wengi zaidi wapate matibabu ya macho kwa faida taifa kwa ujumla,” alisema Dkt.Adubango.
Alisema kampeni hii itaendelea kwenye shule za awali ambapo watoto wa rika la chini ya miaka mitano linapopatikana, hivyo ushirikiano unahitajika kutoka kwa wazazi ili watoto wengi waweze kupatiwa matibabu.
“Katika zahati ya mbande jumla ya watoto 65 wamepimwa macho na kupatiwa matibabu ambapo tatizo kubwa lililoonekana kwa watoto wengi ni alegi ya macho na makengeza ,” alisema Dkt.Adubango.
Alisema wananchi waendelee kujitokeza kwa wingi ili waweze kupatiwa matibabu kwani yanatolewa bure hivyo pale watakaposikiana CCBRT wanatoa huduma wajitokeze wapatiwe matibabu.
Kwa upande wake Mtabibu wa meno zahanati ya Mbande kata ya Chamanzi, Agneta John alisema tunashukuru CCBRT kuleta huduma ya upimaji macho katika zahanati hiyo na kuomba huduma hiyo iendelee kutolewa mara kwa mara ili wananchi wa maeneo hayo na wilaya za karibuni wapate huduma hiyo muhimu.
“Zahanati yetu inatoa huduma ya upimaji wa macho, hivyo na kwa uwepo wa CCBRT ambayo inavifaa vya kutosha tutaweza kuwafikia wagonjwa wengi zaidi na kupelekea kupunguza tatizo la macho nchini,” alisema Agneta.
Zawadi Rajabu mkazi wa Mbande kisiwani mara baada ya mtoto wake kupatiwa matibabu ambayo yanatolewa bure na CCBRT alishukuru na kusema tatizo la mtoto wake limebainika na amepatiwa matibabu.
“Niwaombe watanzania wenzangu tujitokeze kupeleka watoto wetu wakapimwe macho kwani macho ndiyo kila kitu katika maisha ya mwanadamu hivyo tuwatoe watoto wetu wenye matatizo ya macho wapatiwe matibabu ambayo ni bure,” alisema Rajabu.
Kampeni hiyo ya utoaji wa huduma yta matibabu ya macho kwa watoto chini ya miaka mitano inatolewa na Hospitali ya CCBRT kwa ufadhili wa Light for the World.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua