Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online,Dodoma
HOSPITALI ya CCBRT imeahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha afya za Watanzania na hasa kupunguza vifo vya kina mama wakati wa kujifungua.
Hayo yamesemwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa hospitali hiyo, Brenda Msangi wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alipotembelea banda la hospitali hiyo kabla ya kufunga Mkutano wa Mwaka wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO)uliofanyika jijini Dodoma mwishoni mwa wiki.
Brenda amesema hospitali hiyo imeamua kuunga kwa vitendo kauli ya Rais Samia aliyoitoa wakati akihutubia Bunge ambapo katika sekta ya afya alisisitiza kuwa moja ya kipaumbele chake kikubwa ni kupunguza vifo vya mama wakati wa kujifungua.
“Sisi kama CCBRT tunafanya kazi kwa karibu sana na timu ya mkoa ya afya ya Mkoa wa Dar es Salaam. Kwa kipindi cha miaka 10 tumeweza kufanya kazi na vituo 22 vya afya vya Serikali na tumeweza kupunguza vifo vya kina mama kwa asilimia 47,”amesema.
Lakini pia, Brenda amesema CCBRT inatarajia kufungua jengo maalum litakalokuwa likitoa huduma ya uzazi na kujifungua ambalo litakuwa na vitanda 200.
Wakati huo huo, Mtendaji Mkuu huyo pia ameishukuru Serikali kwa kutambua na kuthamini mchango wao baada ya kuibuka mshindi wa kwanza katika Mashirika yasiyo ya kiserikali yaliyoajiri zaidi na kusema kuwa cheti hicho kimewapa motisha sana wa kuendelea kuwahudumia Watanzania.
Amesema ushindi huo wa CCBRT ni kielezo kuwa Serikali na watanzani kwa ujumla wake wanatambua mchango wa hospitali kwa kujali na kuthamini afya za akina mama na mtoto.
‘Sisi kama CCBRT tutaendelea kutoa mchango stahiki katika sekta ya afya sambamba na malengo na matarajio ya Serikali,” amesema.
Katika sherehe hizo hapa, CCBRT ilivutia watu wengi waliotaka kujua huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo muhimu hapa nchini.
More Stories
Madaktari bingwa wa Samia watua Rukwa
Utashi wa Rais Samia na matokeo ya kujivunia vita dawa za kulevya nchini
Uwekezaji wa Rais Samia sekta ya afya waendelea kuwa lulu Afrika