Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online DSM
CHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimewataka walimu na wafanyakazi wa chuo hicho kuboresha huduma kwa wateja na kujiandaa kutoa mafunzo kidijitali ili kuendana na ongezeko kubwa la wanafunzi linalokua mwaka hadi mwaka.
Hayo yamesemwa jana jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Edda Lwoga, wakati akizungumza kwenye kuhitimisha wiki ya huduma kwa wateja chuoni hapo.
Amesema mwaka wa masomo ulioisha walidahili wanafunzi 6,159 kwa Kampasi ya Dar es Salaam lakini kwa mwaka huu wa masomo, kampasi hiyo imefanikiwa kudahili kufikia 15,000.
Profesa Edda amesema kwa Kampasi za Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya na Mwanza idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa imeongezeka wamedahiliwa jumla ya wanafunzi 23, 281
Amesema kutokana na ongezeko hilo la wanafunzi, walimu wa chuo hicho wanawajibika kuboresha huduma wanazotoa kwa kiwango cha juu ili kuendana na ongezeko hilo la wanafunzi.
“Hii inamaana kama ulikuwa unafundisha wanafunzi 200, idadi inaweza kuongezeka ukawa unafundisha wanafunzi 400, kila program sasa hivi tukiangalia imejaa wanafunzi kwa mfano program ya Metrology ambayo mwaka jana tulidahili wanafunzi 40 mwaka huu tumedahili wanafunzi 200,” amesema
Amesema chuo hicho kimeendelea kupanuka na kuipongeza Idara ya Masoko kutokana na jitihada kubwa wanazofanya kutangaza program za chuo.
Amesema mbali na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi, chuo hicho kimeendelea kupanua miundombinu yake kwa kujenga jingo la orofa 10 lenye thamani ya shilingi bilioni 22.4.
Profesa Edda amesema jengo hilo litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kuhudumia wanafunzi 4,200 na aliwataka watumishi wa chuo hicho kuboresha huduma ili ziendane na ongezeko la wanafunzi.
“Tujitahidi kuanza kutoa elimu kwa njia ya mtandao, walimu wanaofundisha program za uzamili na Post Graduate mjiandae kufundisha kidijitali kwenye upande wa Utawala, Rasilimali Watu, Masoko, Biashara Kimataifa na Usimamizi wa Biashara, “ amesema
Profesa Edda amesema chuo kinapaswa kujiandaa kuhudumia ongezeko la wanafunzi kutoka nje ya nchi kwani wamekuwa wakipata wanafunzi kutoka nchi za Comoro, Congo DRC na mataifa mengine Afrika.
Amesema mbali na kutoa huduma bora kwa wateja, wafanyakazi wa chuo hicho wanatakiwa kutoa huduma bora wanapohudumiana wenyewe kwa wenyewe kwa kuhakikisha hakuna malalamiko.
“Sitapenda kusikia malalamiko ya wafanyakazi kwamba nimeenda kwa mtumishi flani faili langu halijatoka, usikae na faili la mtu kwa muda mrefu. Kabla hatujamnyooshea mwingine kidole tuanze kujiangalia kwanza je tunahudumiana ipasavyo na kwa wakati?” alihoji Profesa Edda.
Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Emmanuel Munishi, amesema CBE imekuwa ikisherehekea wiki ya huduma kwa mteja kwa mwaka wa pili sasa ambapo amekuwa wakikutana na kufanya tafakari kuangalia walikotoka, walipo na wanapoelekea.
Amesema lengo la kutafakari ni kuangalia pale ambapo wamefanya vibaya na kufanya maboresho na kuenzi yale mazuri ambayo wamekuwa wakiyafanya kwenye kuhudumia wateja wao.
Amesema kwa mwaka wa masomo uliopita chuo kilifanya vizuri kwenye maeneo tafiti, kufundisha na kutoa ushauri wa kitaalalamu na kwamba idadi ya machapisho yanayotolewa na wataalamu wa chuo hicho imeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka.
Amesema huduma kwa wateja inapaswa kuwa kipaumbele namba moja na kuwataka wale ambao wamekuwa wakifanyakazi kwa mazoea kubadilika.
“Tunaomba tuboreshe mawasiliano ya sisi kwa sisi kwasababu huduma kwa wateja ni pamoja na sisi wenyewe. Mtu ukipewa kazi ukashindwa kuikamilisha toa taarifa kwamba nimefanya mpaka hapa na ukifanya vizuri ukamaliza toa taarifa pia kwamba nimekamilisha,” amesema
“Kama wewe ni mhasibu unajua unatakiwa kufanya malipo unakuta idara haina fedha badala ya kuutarifu uongozi wewe unakaa kimya, mtu wa admission na registration ya wanafunzi unakuta mfumo haufanyi vizuri umekaa kimya na wale wanaosubiri kuhudumiwa wanaendelea kuhangaika,” amesema
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa