Na Martha Fatael, TimesMajira Online
Taasisi ya Climate Action Network (CAN) Tanzania imetaka ahadi za kisiasa za kimataifa kugeuzwa haraka kuwa vitendo vya utekelezaji, huku ikionyesha wasiwasi mkubwa kuhusu mabadiliko yanayoikumba Mlima Kilimanjaro, tegemeo la maelfu ya Watanzania.
Katika maandalizi kuelekea Mkutano wa 30 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP30), unatarajiwa kufanyika Belem, Brazil, Meneja Uendeshaji wa CAN Tanzania, Boniventure Mchomvu, amesisitiza kwamba mkutano huo unapaswa kupeleka mbele umuhimu wa kuweka mifumo ya kusimamia utekelezaji wa makubaliano yaliyopita.
Mfuko wa Fidia na Pengo Kubwa la Fedha Mchomvu, akionyesha msimamo wa CAN, amesema matarajio makuu ni kuona mfuko wa hasara na uharibifu (Loss and damage fund) ukijazwa na kuanza kutoa misaada kwa jamii zinazoathirika na majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi.
CAN inashinikiza mabadiliko ya kimfumo katika ufadhili wa tabianchi, ambapo fedha za kukabiliana na mabadiliko haya zipewe kipaumbele na zisichukuliwe kama kitu cha ziada au kutolewa kama mikopo kwa nchi zinazoendelea.
CAN imeeleza wasiwasi mkubwa kuhusu pengo la kifedha. Ripoti ya UNEP ya mwaka 2024 inathibitisha kwamba mahitaji ya kifedha kwa nchi zinazoendelea (Tanzania ikiwemo) ni Dola za Kimarekani bilioni 387 kila mwaka hadi kufikia mwaka 2030, huku kiasi halisi cha fedha za umma za kimataifa zilizotolewa mwaka 2022 kikiwa Dola za Kimarekani bilioni 27.5 tu.
Pengo hili linaikwamisha nchi kutekeleza kikamilifu mipango yake ya Kitaifa.Sauti Kutoka Kilimanjaro:
Uhai Upo HatianiKatika Mikoa ya Kaskazini mwa Tanzania, hasa Kilimanjaro,
sauti za wananchi na wadau zinasisitiza haja ya fidia ya kimazingira na hatua za haraka, kufuatia kasi ya kuyeyuka kwa barafu ya Mlima Kilimanjaro ambapo wakazi hao, hususan katika vijiji vya Marangu, Mwika, na Uru Mashariki (Wilaya ya Moshi), wakiendelea kushuhudia athari za kuyeyuka kwa barafu, wanataka hatua za dharura zichukuliwe ili kulinda vyanzo vya maji vinavyotegemewa na jamii nyingi kwa matumizi ya nyumbani, kilimo, na mifugo.
Rehema Mosha, mkazi wa kijiji cha Marangu Mtoni, anasema upungufu wa maji umeathiri shughuli za kilimo cha kahawa na ndizi ambavyo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa eneo hilo kwani mito mingi imeanza kukauka hivyo tunahitaji miradi ya uhifadhi wa misitu na upandaji miti ifanyike sasa, si kesho.
Naye Leonard Kimaro kutoka Mwika, anasisitiza kwamba jamii zinazoathirika moja kwa moja zinapaswa kupewa kipaumbele katika mgao wa fedha za Mfuko wa Hasara na Uharibifu, kwa kuwa ndizo zenye mzigo mkubwa wa athari za mabadiliko ya tabianchi.
Wakazi wengine, kutoka wilaya ya Hai wakiwemo wale wa vijiji vya Kirua Vunjo Kusini na Machame, wanasema wanahitaji elimu endelevu kuhusu mabadiliko ya tabianchi na mbinu bora za kukabiliana nazo, hasa katika sekta za kilimo na maji ambazo ndizo nguzo kuu za uchumi wao.
Juliana Shayo, mkulima kutoka Machame, anasema uelewa mdogo wa wananchi kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi umekuwa ukichangia uharibifu wa mazingira, ikiwemo ukataji miti na matumizi yasiyo endelevu ya ardhi.Mkuu wa Sekta ya Sayansi Asilia wa UNESCO, Keven Robert, amesema barafu ya mlima huo imepungua zaidi ya asilimia 80 katika kipindi cha karne moja iliyopita.
Wataalamu wa serikali wameeleza kuwa kuyeyuka kwa barafu ni kiashiria cha maisha ya maelfu ya Watanzania Afisa Mazingira Mwandamizi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Makuru Nyarobi, ametoa mfano wa Mlima Kilimanjaro, akisema kuyeyuka kwa barafu kunatishia vyanzo vikubwa vya maji, utalii, na kilimo.
Dkt. Nyarobi anasisitiza hoja ya Afrika kuwa mataifa makubwa yanapaswa kuwajibika zaidi kwa sababu hayakuchangia sawa kwenye uzalishaji wa gesijoto, akibainisha: “Sisi tunaona wao wanaowajibu wa kufanya zaidi maana wamechangia zaidi kwenye changamoto… kimsingi hatuwezi kuwajibika sawa maana hatukuharibu sawa”.
Vipaumbele Vingine vya CAN kuelekea COP30, CAN inatarajia kuona ongezeko la ufadhili wa kimataifa ukilenga miradi mikubwa ya nishati mbadala nchini Tanzania, kama vile nishati ya jua, upepo, na jotoardhi. Pia wanataka makubaliano ya kimataifa yalete fedha za kutosha za kuimarisha programu za kitaifa za uhifadhi wa misitu ya asili, maeneo oevu, na vyanzo vya maji.
CAN inafanya kazi kwa karibu na Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) kuandaa Msimamo Jumuishi wa Taifa. Shirika hilo liliandaa vikao vya kitaalamu (Pre-COP30 Technical Sessions) kuhakikisha maoni ya vijana, wanawake, na asasi za kiraia yanaingizwa moja kwa moja kwenye ajenda ya Kitaifa.
CAN pia itatuma wawakilishi wawili kuhudhuria COP30 nchini Brazil ili kushinikiza utekelezaji wa ahadi za kutoa fedha na kuhakikisha sauti za jamii zilizo hatarini zaidi zinasikika.Ili kufikia malengo hayo, CAN inasisitiza haja ya kurahisisha mchakato wa upatikanaji wa fedha, kwa kuwa taratibu za kuzipata ni ngumu, zenye masharti magumu, na zinachukua muda mrefu.
Pia inahitajika kuongeza uwezo wa kitaasisi na kiufundi katika ngazi za wilaya na vijiji katika kuandaa, kuandika, na kusimamia miradi ya mabadiliko ya tabianchi inayoweza kuomba ufadhili kimataifa

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama