January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bweni la shule ya sekondari Ziba lateketea kwa moto

Na Lubango Mleka, Times majira online – Igunga.

BWENI la wanafunzi wa kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari Ziba iliyopo kijiji cha Ziba, Kata ya Ziba Wilaya ya Igunga mkoani Tabora limeteketea kwa moto majira ya saa tatu asubuhi Januari 23,2024 na kuteketeza baadhi ya vitu ikiwemo vitanda, magodoro na vifaa vya wanafunzi.

Akizungumzia tukio hilo Diwani wa Kata hiyo Salawa Maganga Mayunga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa alipigiwa simu majira ya saa tatu asubuhi na alipofika alikuta juhudi za kuokoa mali zikiendelea ambapo wameokoa baadhi ya masanduku na magodoro ya wanafunzi.

Ambapo ameeleza kuwa zaidi ya wanafunzi 212 ambao wanatumia bweni hilo walikuwa darasani wakati tukio hilo linatokea.

“Ni kweli bweni la shule yetu ya sekondari Ziba limeteketea kwa moto, , bahati nzuri kikosi cha Zimamoto kutoka Nzega walipigiwa simu na kufika baada ya nusu saa na kukuta bweni lote limeshika moto na kuanza juhudi za haraka kuuzima,” amesema.

Ameendelea kusema kuwa, wameokoa magodoro 48, masanduku ya kutunzia mali za wanafunzi 13 huku mengine yakiteketea kwa moto.

” Chanzo cha moto bado hatujajua kwani wanafunzi wote walikuwa darasani na waliona moshi ukitoka juu ya paa la bweni hilo lijulikanalo kwa jina la Gulamali walikwenda na kukuta moshi umesambaa ndani ya bweni lote hivyo kushindwa kuungia ndani na kuokoa mali mpaka hapo ilipopigwa simu kwa kikosi cha Zimamoto Nzega,”amesema Mayunga.

Ametoa wito kwa wadau wa elimu, mtu binafsi,benki na taasisi mbalimbali kuguswa na tukio hilo na kutoa michango yao ya dharura ikiwa ni pamoja na magodoro, vifaa vya shule kwa wanafunzi ambao vifaa vyao vimeteketea kwa moto ili waweze kuendelea na masomo.

Mkuu wa Wilaya ya Igunga Sauda Mtondoo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ametafutwa kwa njia ya simu na kuhaidi kuzungumzia tukio la kuungua kwa bweni atakapo toka kwenye kikao cha kujadili tukio hilo