December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bunge lapitisha azimio la kumpongeza Rais Magufuli

Na Doreen Aloyce, TimesMajira Online, Dodoma

BUNGE la Jamhuri wa Tanzania limepitisha kwa kishindo azimio la kumpongeza Rais John Magufuli kwa kupambana na ugonjwa wa Corona nchini Tanzania.

Wakichangia kwa nyakati tofauti wabunge wa mbalimbali wamesema kitendo alichokifanya Rais Magufuli ni mfano wa kuigwa katika nchi za jirani na mataifa mengine.

Mbunge wa Jimbo la Hanan’g, Mary Nagu amesema kuwa rais ameipa heshima nchi hii na kuifanya kuwa ya pekee duniani kote ambapo alitumia vizuri vipaji alivyopewa, ambapo kupitia huu ugonjwa wa Corona ameweka jitihada za kuweka hospital ngazi mbalimbali ambazo zimesaidia kukabiliana na ugonjwa huu.

Nagu amesema kuwa kupitia ugonjwa huo Rais Magufuli aliwaondoa hofu wananchi na kuzuia kuendelea kujifungia ndani jambo ambalo limewafanya Watanzania kufanya kazi kwa bidii huku wakipata mahitaji yao na kuinua uchumi wa taifa tofauti na nchi nyingine ambazo walijifungia .

Ameongeza kuwa katika jitihada za  rais alihakikisha anahamasisha watu kusali na kumtegemea Mungu jambo ambalo liliwafanya watumishi wa Mungu na jamii kwa ujumla kumtegemea Mungu badala ya kujikinga kwenye miungu mingine na kupelekea ugonjwa huo kupungua kwa kiasi kikubwa .

Amesema kuwa Rais Magufuli amekuwa mfano bora kwenye taifa kupitia ugonjwa huo kwani kila alichokitamka hata mataifa mengine walimuiga na kufuata maelekezo yake jambo ambalo lilionesha ni kiasi gani rais ni kiongozi wa mfano.

Nae Mbunge wa Jimbo la Nkasi Ally Kesi amelitaka bunge kumuongezea muda Rais John Magufuli wa kuendelea kuliongoza taifa kwa miaka mingine baada ya kumaliza kipindi hiki kwani amekuwa kiongozi bora.

Kesi amesema “kwa kazi aliyoifanya rais, atake asitake atalazimishwa tu aendelee kuongoza nchi kwani kitendo cha Corona kila nchi imeiga mfano wake.”

Akijibu mchango huo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amesema, kwa sasa bunge haliwezi kutoa maamuzi kwani bado mchakato wa uchaguzi katika awamu ya pili haijaisha na kumtaka mbunge huyo kusubiri baada ya awamu hii.

“Sisi ndiyo wenye mamlaka hivyo baada ya uchaguzi mkuu wakirudi watakaoliongelea Bungeni kwani hilo suala liko ndani ya uwezo wetu wa kutaka asitake atalazimishwa tu hivyo Mheshimiwa Kesi nikutake utulie na hoja yako mpaka tutakaporejea Oktoba “alisema Spika

Amesema kitendo cha Rais John Magufuli kuwaunganisha Wakristo na Waislamu kusali kwa pamoja na jambo hilo limefanikiwa na kudai Rais ametetea uhuru wa Watanzania kwa vitendo.