Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Korogwe
KAMATI ya Ardhi, Maliasili na Utalii, imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kusikiliza kilio cha wananchi kuhusu wanyama wakali na waharibifu na kuwajengea vituo na kutoa vifaa vya kukabiliana na changamoto hiyo katika maeneo mbalimbali nchini.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Timotheo Mnzava, alitoa shukrani na pongezi hizo leo wakati kamati hiyo ilipokuwa ikihitimisha ziara yake ya siku tatu katika Mkoa wa Tanga kukagua mradi mbalimbali.
Jana Kamati hiyo ilikagua ujenzi wa kituo maalum cha kukabiliana na tembo kilichokamilika kwa asilimia 100 katika kijiji cha Goha kata ya Mkumbara, wilayani Korogwe.
“Tumeridhishwa na kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Rais wetu kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii katika kukabiliana changamoto hii katika kipindi kifupi, kwa niaba ya kamati naomba nimshukuru na kumpongeza sana” alisisitiza Mnzava
Kituo hicho ambacho kimetumia sh. milioni 48 kukamilika pia Serikali imetoa vifaa yote muhimu ikiwa ni pamoja na samani, ndege nyuki moja , gari moja na askari sita ambao watakuwa kituoni hapo wakati wote.
Kituo hicho ambacho kina vyumba vikubwa vitatu, Ofisi moja, jiko, bafu na choo kitasaidia kukabiliana na changamoto hiyo katika vijiji zaidi ya kumi vinavyovunguka eneo hilo.
Baadhi ya vijiji vitakavyofaidika moja kwa moja na kituo hiki ni pamoja na Manga, Mtitiro, Masira, Kwenangu, Mkomazi na Mikochen imeeleza taarifa ya Hifadhi ya Ngorongoro, taasisi ambayo imepewa jukumu la kujenga na kusimamia.
Aidha, Mnzava aliitaka Wizara kuhakikisha mara baada ya kukamilisha vituo hivyo kuleta vifaa yote muhimu na watumishi wanaohitajika na wawepo muda wote.
Kamati hiyo iliambatana na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula, Katibu Mkuu, Dkt. Hassan Abbasi, Naibu Katibu Mkuu, Kamishina wa Polisi, Benedict Wakulyamba na watendaji kutoka wizarani na kwenye taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo
More Stories
Dkt.Mpango aipongeza STAMICO kuwa mfano bora utekelezaji matumizi nishati safi ya kupikia
Wezi wa mapato manispaa Tabora kukiona cha moto
Uwindaji wa kitalii kuingizia Tanzania Bil.2.5