June 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bumbuli wamshukuru Rais Samia kwa miradi ya maji

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Bumbuli

BAADHI ya wananchi wa Kijiji cha Funta, Kata ya Funta, Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli (Bumbuli DC) iliyopo Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga wamemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea mradi wa maji.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Juni 10, 2025 wakati wa mapokezi ya Mwenge wa Uhuru, ambapo Mwenge wa Uhuru ulizindua Mradi wa Maji Funta, walisema mradi huo umewaondoa kwenye mateso, kwani walikuwa wanakwenda kutafuta maji kwenye vidimbwi, huku wakichukua muda mrefu kupata maji hayo.

“Tulikuwa tunapata shida ya maji kwa kwenda umbali mrefu kutafuta maji hayo. Ni afadhali yangekuwa mengi, lakini yalikuwa ni maji kidogo yaliyopo kwenye vidimbwi, na mnasubiriana kwa muda mrefu kupata maji hayo, wakichota wawili au watatu yanakata, inabidi msubiriane yaweze kujaa tena ndiyo mchote.

“Unarudi nyumbani ni ugomvi sababu ya kuchukua muda mrefu kwenye kutafuta maji. Sasa hivi hata mifugo inafurahi sababu inakunywa maji mengi hadi ndoo mbili, lakini zamani ilikuwa inakunywa nusu kindoo. Sasa hivi sisi tunafurahi na wanyama wetu wanafurahi, hivyo tunaishukuru sana RUWASA, na tunamshukuru Rais wetu Dkt. Samia kwa kutuletea mradi huu wa maji” amesema Faudhia Adam, mkazi wa Kijiji cha Funta.

Naye Saumu Ngwilizi amesema wanamshukuru Rais Dkt. Samia pamoja na Mbunge wa Jimbo la Bumbuli January Makamba kwa kuweza kuwaletea mradi wa maji, kwani kwenye Zahanati ya Funta walikuwa hawana maji, lakini kwa ujio wa mradi huo kwa sasa tatizo hilo limekwisha, na wanawake wanaojifungua hapo wanakuwa salama zaidi hasa kwenye suala la usafi.

“Tunamshukuru Mama Samia pamoja na Mbunge wetu January Makamba, wameweza kutuletea huduma ya maji, na sasa hivi hata hospitali (Zahanati) yetu ya Funta ina maji. Zamani ilikuwa mwanamke akijifungua usiku, wasaidizi wake wanakwenda kutafuta maji mabondeni, tena usiku, lakini kwa sasa tatizo hilo limekwisha” alisema Ngwilizi.

Sophia Mtunguja amesema wamefurahi kupata huduma ya maji, kwani ilikuwa ni changamoto kubwa kwenye kijiji chao, kwani walikuwa wanapata shida ya maji kuanzia kwenye nyumba zao hadi Zahanati ya Funta, lakini sasa hivi wana maji, lakini pia wana umeme, hivyo wanatoa shukrani nyingi kwa Rais Dkt. Samia.

Naye Mbunge wa Jimbo la Bumbuli January Makamba akizungumza mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ismail Ali Ussi, amesema Mwenge wa Uhuru unakwenda kwenye vijiji ambako maendeleo yamefanyika, hivyo wananchi wa Funta, na maeneo ya vijiji vya Jimbo la Bumbuli, kuna maendeleo yamefanyika.

“Mwenge umekuja kuzindua mradi wa maji, na katika halmashauri yetu leo kutwa nzima tunapita tukizindua miradi mbalimbali. Hii miradi tafsiri yake kuna mambo ya maendeleo yamefanyika kwenye halmashauri yetu, ingekuwa hakuna mambo ya maendeleo tusingekuwa na la kufanya, na Mwenge ungekuwa hauna kazi, tungekuwa tu tunaukimbiza barabarani.

“Lakini tunasimama, na pia mjue, kuna miradi mingi tumeiacha sababu ya muda, ingekuwa kila mradi uliofanyika uzinduliwe na Mwenge, Mwenge usingeondoka Bumbuli siku tatu, lakini tulichagua… maana yake nini, ni kwamba kuna mambo yamefanyika. Sasa, yakifanyika mambo ya maendeleo, kuna mkono ulioyawezesha. Mkono wa kwanza ni Chama Cha Mapinduzi, sababu mambo yote yanayofanyika yanatokana na Utekelezaji wa Ilani ya CCM (2020-2025, na ahadi za Chama Cha Mapinduzi kwa wananchi. Mradi huu hapa leo ni Utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi” amesema Makamba.

Kabla ya kuzindua mradi huo, Ussi alipongeza Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa kujenga mradi huo, kwani kwa mazingira ya milima na mabonde, watu wengine wasingeweza kufanya kazi hiyo.

“Tumekuja hapa tumejionea mambo mazuri, mambo makubwa, lakini pia tumefika hapa eneo la Funta kwa kweli yaliyofanyika hapa ndugu zangu wananchi, kwa kweli hayawezi kufanyika maeneo yeyote mengine zaidi ya eneo la Funta. Na kutokana na taarifa iliyotolewa hapa, wananchi walikuwa na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama, lakini kwa vile Serikali yao ni sikivu, imeweza kuwaletea mradi wa maji safi na salama, na tumeona, manufaa yake ni makubwa” amesema Ussi.

Akisoma taarifa ya Ujenzi Mradi wa Maji Funta, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin Sizinga amesema ujenzi wa miundombinu ya maji katika mradi wa Funta ni miongoni mwa miradi ya maji inayoendelea kutekelezwa na Ofisi ya Menaja wa RUWASA Lushoto kupitia fedha za
Mfuko wa Maji.

“Mradi huu unatekelezwa na Mkandarasi MS KOBERG CONSTRUCTION
COMPANY LIMITED WA DAR ES SAAAM KWA Mkataba Namba AE-
102/2021-2022/TAG/W/61 Kiluwai – Kidundai, Funta na Wanga wenye thamani ya sh. 2,702,000,937. Utekelezaji wa kazi kwa eneo la Funta ulianza rasmi Agosti 18, 2022 na unategemea kukamilika Juni 30, 2025. Mradi huu unatarajiwa kuhudumia wananchi 4,782 wanaoishi katika Kijiji cha Funta na Kijiji cha Manga

“Kazi zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa tenki la lita 120,000 ambalo ujenzi wake umekamilika asilimia 100, uchimbaji wa mtaro mita 1,300 za Bomba kuu (Gravity main), uchimbaji wa mtaro mita 9,527 za distribution lines  ulazaji wa bomba, ujenzi wa vituo vya maji 23, ujenzi wa Cum-Storage tanks tano zenye ujazo wa lita 1,000 vyote vimekamilika kwa asilimia 100” amesema Mhandisi Sizinga.

Mhandisi Sizinga amesema mradi huo unagharimu sh. 832,655,200. Mkandarasi yupo eneo la kazi (Site) anaendelea na ukamilishaji wa kazi maeneo mengine. Mpaka sasa
Mkandarasi amelipwa sh. milioni 651, na kwa sasa mradi umekamilika asilimia 100.

“RUWASA tunatoa shukrani za dhati kwa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kuendelea kutupatia fedha za miradi ya maendeleo, tutazisimamia vizuri ili ziweze kuleta tija kwa wananchi na kufikia malengo yaliyokusudiwa” alisema Mhandisi Sizinga..