December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Breaking: Wabunge 69 CHADEMA waitwa kuhojiwa TAKUKURU

Na Mwandishi Wetu

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Makao Makuu, imewaita wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na waliowahi kuwa wabunge wa chama hicho kwa ajili ya mahojiano.

Taarifa iliyotolewa na TAKUKURU leo asubuhi imeeleza kuwa hatua hiyo inafanyika ikiwa ni mwendelezo wa uchunguzi unaoendeshwa na TAKUKURU Makao Makuu kuhusiana na malalamiko dhidi ya matumizi ya fedha za CHADEMA, ambapo hatua iliyopo sasa ni ya kuwahoji wabunge  69, wanachama na waliowahi kuwa wanachama wa chama hicho.

Fedha hizo ni zile ambazo zililalamikiwa na waliokuwa wabunge wa chama hicho ambao walitangaza kukihama chama chao ambapo katika malalamiko yao, walidai kwamba walikuwa wakikatwa fedha katika mishahara yao kila mwezi kuanzia Juni 2016.

Kwa mujibu wa malalamiko hayo kila mwezi — wabunge wa Viti Maalum walikuwa wakikatwa kiasi cha sh. 1,560,000 na wale wa kuchaguliwa kwenye majimbo walikuwa wakikatwa sh. 520,000 na kwamba hawakuwa wakifahamu namna ambavyo fedha hizo zimekuwa zikitumika.

“Kwahiyo, tunapenda kuujulisha umma kwamba, kama ambavyo Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Brigedia Jenerali John Mbungo alivyoviambia vyombo vya habari Mei 27, 2020 ni kwamba uchunguzi dhidi ya tuhuma hii tayari ulisha anzishwa na baadhi ya wahusika walishaanza kuhojiwa,” imeeleza taarifa hiyo