March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

BREAKING: Spika Mstaafu Job Ndugai afariki dunia jijini Dodoma

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dodoma

TANZANIA imempoteza mmoja wa wanasiasa wake mashuhuri na kiongozi aliyelitumikia Bunge kwa muda mrefu, Mheshimiwa Job Yustino Ndugai, aliyefariki dunia leo asubuhi jijini Dodoma akiwa na umri wa miaka 62.

Taarifa rasmi ya kifo hicho imetolewa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Tulia Ackson, ambaye alieleza masikitiko yake makubwa kutokana na kuondokewa na kiongozi aliyeacha alama isiyofutika katika historia ya Bunge la Tanzania.

“Kwa masikitiko makubwa, naomba kutoa taarifa ya kifo cha kiongozi wetu, mwanasiasa mkongwe na Spika Mstaafu wa Bunge, Job Yustino Ndugai kilichotokea leo jijini Dodoma. Natoa pole kwa familia ya Marehemu, ndugu, jamaa na Wananchi wa Jimbo la Kongwa, Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu,” alisema Spika Tulia Ackson kupitia taarifa rasmi kutoka Ofisi ya Bunge.

Kwa sasa, mipango ya mazishi ya kiongozi huyo inaratibiwa na Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na Kamati ya Mazishi pamoja na familia ya marehemu, na taarifa zaidi zitatolewa kadri mipango itakavyokamilika.

Historia Fupi ya Job Ndugai

Marehemu Job Yustino Ndugai alizaliwa tarehe 22 Januari, 1963. Amekuwa Mbunge wa Jimbo la Kongwa, nafasi aliyoshikilia kwa vipindi kadhaa mfululizo, akijijengea heshima kama mwakilishi wa wananchi mweledi na mwenye maono.

Alitumikia pia kama Naibu Spika kabla ya kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015, nafasi aliyohudumu hadi alipojiuzulu mwaka 2022. Katika kipindi chake kama Spika, Ndugai alijulikana kwa msimamo wake wa kulinda heshima ya Bunge, nidhamu kwa wabunge, na usimamizi wa mijadala ya kitaifa kwa umakini na weledi wa hali ya juu.

Zaidi ya siasa, marehemu Ndugai alikuwa mtumishi wa umma aliyebobea katika sekta ya elimu na maendeleo ya jamii, akiwa na shahada kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mafunzo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.

Kifo chake kinakuja wakati taifa likiendelea kuimarisha misingi ya demokrasia, utawala bora, na maendeleo ya kisekta—mambo ambayo aliyapigania kwa juhudi kubwa akiwa Bungeni.

Rambirambi zimeendelea kumiminika kutoka kwa viongozi wa serikali, vyama vya siasa, wabunge, viongozi wa dini, na wananchi wa kawaida walioguswa na kifo hicho cha ghafla.

Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.