December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Revocatus Malimi

BREAKING: Polisi waua watuhumiwa saba wa ujambazi Kagera

Na Ashura Jumapili, TimesMajira Online, Biharamulo,

JESHI la Polisi mkoani Kagera limefanikiwa kuwaua watu saba wanaodhaniwa kuwa majambazi waliokuwa wanajiandaa kuteka magari na kupora wakiwa na silaha ya kivita AK 47, risasi na bomu la kurushwa na mkono wilayani Biharamulo mkoani humo.

Akiongea na waandishi wa habari jana Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Revocatus Malimi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo jana, mwaka huu saa 7.30 usiku eneo la Nyamalagala Tarafa ya Rusahunga Wilaya ya Biharamulo Barabara Kuu iendayo Wilayani Ngara.

Kamanda Malimi, amesema Polisi lilipambana na kufanikiwa kuwaua watu saba wanaodhaniwa kuwa majambazi waliokuwa wanajiandaa kuteka magari na kupora .

Amesema wakati wa upekuzi eneo la tukio kumepatikana bunduki ya kivita moja aina ya AK 47 ambayo imefutwa namba, risasi 11 zikiwa ndani ya magazine na bomu moja la kutupa kwa mkono.

Amesema, awali jeshi hilo lilipata taarifa kutokea kwa wananchi baada ya kuona kikundi cha watu wasiowatambua na wakati huo wakapata taarifa kuwa ni majambazi waliokuwa wanajiandaa kufanya utekaji Wa magari ndio wakatoa taarifa Polisi.

Amesema Polisi baada ya kupata taarifa kupitia kikosi kazi chake maalum kiliandaa mtego na hatimaye jana usiku walifanikiwa kuwaweka katikati ya mtego, lakini majambazi yalipogundua yemeingia kwenye mtego yalianza kufyatua risasi hovyo.

“Polisi walijibu kwa ujasiri na kufanikiwa kuwapiga risasi ambazo ziliwajeruhi na hatimaye kusababisha vifo vya watu saba wa jinsia ya kiume wenye umri kati miaka 25-35 ambao hadi sasa hawajatambuliwa,” amesema kamanda Malimi.

Amesema miili yao imehifadhiwa katika Hospitali ya Biharamulo ikisubiri kutambuliwa. Kamanda Malimi alitoa shukrani kwa wananchi waliotoa taarifa na kuwataka waendelee kufanya hivyo ili jeshi la Polisi liendelee kuweka amani na utulivu katika mkoa huo.