January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

BREAKING NEWS:Wizara ya Maliasili yatumbua vigogo wake, wengine wasimamishwa kupisha uchunguzi

Na Mwandishi Maalum, TimesMajira Online

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali chini ya Wizara ya Fedha na Mipango baada ya kufanya ukaguzi maalum kwenye Mfukowa Maendeleo ya Utalii (TDL) imebaini ubadhirifu mkubwa katika mfuko huo na imechukua hatua za haraka.

Hayo yamebainishwa na Msemaji wa wizara hiyo, Dorina Makaya kupitia taarifa aliyoitoa muda huu kwa umma.

Amesema, kufuatia ukaguzi huo, wizara imebaini mapungufu na ubadhirifu mkubwa kwenye mfuko wa TDL.

Makaya ameeleza kuwa, kutokana na hali hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mamlaka aliyonayo amefanya maamuzi haya;

“Ametengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Utalii, Deogratius Mdamuna, kumsimamisha kazi kupisha uchunguzi,pia amemsimamisha kazi Flora Masami, Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa wizara ili kupisha uchunguzi. Mbali na hayo amemwelekeza Kamishna wa Hifadhi za Taifa (TANAPA) kumsimamisha kazi Moses Msemo aliyekuwa Mhasibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii ili kupitisha uchunguzi,

“Pia amemuomba Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kumchunguza Eliud Kijalo aliyekuwa Mhasibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Utalii (TDL), na maofisa wengine ambao wamehusika na ubadhirifu huo. Bwana Kijalo tayari amekamatwa ili kusaidia upelelezi,”amefafanua.

Hata hivyo, wizara hiyo imehaidi kushirikiana na TAKUKURU ili wahusika wote wachukuliwe hatua stahiki na kwa haraka.