Na Issa Mtuwa-WM,Mara
Vifo vya wachimbaji wadogo wawili wa madini na majeruhi nane vilivyotokea katika Kijiji cha Magunga Wilaya ya Butiama vimemfadhahisha Waziri wa Madini, Doto Biteko.
Waliofariki ni Kisambi Daudi (30) Mwikizu, mkazi wa Magunga Wilaya ya Butiama na Marwa Mwita Magige (48) Mkurya mkazi wa Nyaburundu wilaya ya Bunda ambao wamefariki usiku tarehe 11/06/2020 katika mgodi wa Irasaniro Buhemba mkoani Mara.
Ni baada ya kufukiwa na kifusi na kuokolewa wakiwa wamefariki na miili yao imehifadhiwa katika kituo cha Afya Nyamuswa.
Biteko amesema, chanzo vya vifo hivyo ni kutokana na ukaidi wa wachimbaji wadogo kutofuata maelekezo ya wataalamu wa madini.
Amesema, eneo lilitokea vifo hivyo lilizuiliwa na Mkurugenzi wa Migodi nchini, Dkt. Abdruhamani Mwanga kutoka Tume ya Madini aliyetembelea eneo hilo siku chache zilizopita na kuzuia eneo hilo lisichimbwe kabla ya vifo hivyo kutokea.
Biteko ameongeza kuwa, pamoja na katazo hilo wachimbaji hao walikwenda usiku na kuanza kuchimba.
Katika tukio hilo, Mkuu wa Kituo cha Polisi Buhemba Inspekta Maige alijeruhiwa kwa kupigwa na jiwe kichwani wakati akiwatawanya wachimbaji waliokuwa wamekusanyika kwenye eneo hilo kwa ajili ya usalama wao.
Akizungumza kwa ukali na huzuni akiwa mgodini hapo leo, Waziri Biteko amesema, ukaidi wa kutofuata sheria na utaratibu unaotolewa na wataalam wa madini ni tatizo kwa wachimbaji wa madini.
Ameongeza kuwa, endapo wachimbaji hao wasingekaidi maelekezo ya wataalamu madhara hayo yasingetokea.
Anasema, kazi yake kubwa ni kutekeleza anachoagizwa haswa ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali ili fedha hizo zikatatue changamoto ya wananchi na kuleta maendeleo ya watanzania wote.
Amesema, wizara yake siku zote anaongelea kuhusu Namba (takwimu) lakini sio Namba za vifo ndio maana anahuzunishwa na vifo hivyo.
Kufuatia hali hiyo Biteko ametoa maagizo ni marufuku uchimbaji wa madini wakati wa usiku na kuiagiza ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Butiama na kamati ya ulinzi na usalama kuhakikisha uchimbaji wa usiku haufanyiki na atakae kamatwa achukuliwe hatua ya kisheria.
Eneo la mgodi wa Buhemba kumekuwa na matukio ya vifo vya wachimbaji wadogo na machimbo hayo yalishawahi kufungwa kutokana na wachimbaji kufukiwa. Ufunguaji wake uliendana na utekelezaji wa mashariti waliyopewa ingawa vifo hivyo vimetokea eneo jingine, lakini hapo hapo Buhemba.
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Jay-Z aunganishwa na P Diddy kwa kumdhalilisha binti wa miaka 13
Rais Samia afanya uteuzi