December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

BREAKING NEWS: Ajali yaua 25 Arusha

Na. Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Arusha

WATU ishirini na tano (25) wameafariki dunia huku wengine ishirini na moja (21) wakijeruhiwa katika ajali iliyotokea maeneo ya Ngaramtoni Kibaoni ikihusisha lori na magari mengine madogo matatu Wilaya ya Arumeru, Mkoa wa Arusha.

Akitoa taarifa ya ajali hiyo Kamishna wa Polisi Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, CP Awadhi Juma Haji alipofika katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru amesema ajali hiyo ilitokea leo saa 11:00 jioni katika barabara ya Arusha – Namanga ambapo lori lenye namba za usajili KAC 943 H aina ya Mack lenye tela namba za usajili ZF 6778 mali ya kampuni ya KAY Construction ya Nairobi Nchini Kenya.

CP Awadhi ametaja idadi ya waliofariki katika ajali hiyo kuwa ni wanaume (14) wanawake (10) na mtoto mmoja wa kike ambao jumla yao ni (25) huku akiitaja idadi ya raia wa kigeni waliofariki kuwa ni saba (07).

Katika ajali hiyo pia CP Awadhi ametaja idadi ya majeruhi kuwa ni 21 kati yao wanaume ni kumi na nne (14) na wanawake ni saba (07), huku akitaja magari yaliyopata ajali katika tukio hilo kuwa ni T 623 CQF aina ya Nissan Caravan, T 879 DBY aina ya Mercedes Benz Saloon na gari namba T 673 DEW aina ya Toyota coaster mali ya shule ya (New Vision School).

Pia kamishna huyo wa opereshini na mafunzo ya Jeshi la Polisi nchini amekitaja chanzo cha ajali hiyo kuwa kuwa ni kufeli breki ya lori kitendo kilichopelekea lori hilo kuyagonga magari mengine yalikuwa mbele yake huku akibainisha kuwa Jeshi hilo linaendelea kumtafuta dereva aliyesababisha ajali hiyo ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.

Sambamba na hilo ametoa Pole kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha na watanzania kwa ujumla na raia wa kigeni waliopoteza ndugu zao katika ajali hiyo.