Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
SERIKALI imenunua boti kumi za doria zitakazosambazwa maeneo mbalimbali, ikiwemo Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,mkoani Mwanza.Ili kulinda rasilimali za uvuvi katika Ziwa Victoria na kudhibiti uvuvi haramu.
Pia imewezesha miundombinu ya masoko ya kuuzia mazao ya uvuvi likiwemo soko la Kirumba Mwaloni,Kayenze na Igombe,yaliopo Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.Pamoja na soko la Chifunfu wilayani Sengerema na Kigangama Wilaya ya Magu,mkoani humu.
Hayo yameelezwa Agosti,26,2024,na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Riziki Shemdoe, wakati akifungua kikao kazi cha kuhamasisha wadau wa uvuvi kudhibiti uvuvi haramu na biashara haramu ya mazao ya uvuvi Ziwa Victoria.
Amesema licha ya mazao ya samaki kuongezeka nchini,”Bado tunapitia changamoto kadhaa, zikiwamo za uvuvi haramu,uharibifu wa mazalia ya samaki na matumizi ya nyavu za macho (matundu) madogo,makokoro na nyavu za timba,ili kudhibiti uvuvi huo boti kumi zimetolewa na serikali,”ameeleza Profesa Shemdoe. na kuongeza:
“Uvuvi haramu bado ni tatizo,serikali tumeona tuje na mkakati wa kudhibiti uvuvi haramu na biashara ya samaki wachanga hasa sangara, wanaouzwa sokoni bila kuharibu upatikanaji wa samaki.Pia,tuna mpango wa kuweka maboya katika mipaka ya maeneo ya mazalia ya samaki,ili kuwanusuru wakue na kuongezeka ikizingatiwa ulinzi wa rasilimali hizo ni jukumu letu sote,”.
Ameeleza kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye rasilimali za uvuvi (samaki na viumbe hai wengine),inashika nafasi ya kumi Afrika,mwaka 2023 sekta ya uvuvi ilikua kwa asilimia 1.4 na kuchangia asilimia 1.7 ya pato la taifa,pia asilimia 30 ya protini na kutoa ajira milioni 6 mchango ambao si mdogo.
“Ulaji wa samaki uko chini licha ya wingi wa rasilimali ziliopo,takwimu za Shirika la Afya Dunia (WHO), zinatwambia mtu mmoja anatakiwa kula kilo 20 lakini wastani wetu ni kilo 7.6 kwa mwaka.Hivyo ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba utaongeza ulaji wa samaki,”amesema Profesa Shemdoe.
Kwa mujibu wa Profesa Shemdoe mwaka 2024, Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan aligawa vizimba na boti 160 za uvuvi nchi nzima kwa mkopo nafuu, ili kuwawezesha wavuvi wazitumie kuongeza umbali wa kwenda kuvua na kati ya boti hizo 151,zinafanya kazi kwa ufanisi wa asilimia 95 licha ya kuwa mradi huo ni mpya.
Aidha vizimba 222 vilivyotolewa na serikali kwa mkopo,Wizara ina uhakika vitafanya kazi vizuri na itaendelea kuwawezesha vijana na wanawake wakiwemo wazee kujiingiza kipato kwa kufanya ufugaji endelevu wa samaki.Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25, serikali imetenga bilioni 460 ziiwezeshe Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutekeleza mipango ya maendeleo ya sekta ya uvuvi.
Profesa Shemdoe amesistiza kuwa ili kulinda rasilimali ya uvuvi watahamishia mikakati iliyotumika kukomesha uvuvi haramu wa vilipuzi baharini katika Ziwa Victoria, hivyo jamii ya wavuvi,wadau na wananchi wasaidie kuwafichua wahusika wa vitendo vya uvuvi haramu,wakifanya hivyo wataongeza mavuno na mapato ya serikali.
Mkurugenzi wa Uvuvi,Profesa Mohammed Sheikh,amesema mkutano huo umelenga kudhibiti uvuvi haramu kwa kushirikiana na wadau kwa maslahi ya Ziwa Victoria, ili kuwe na agenda ya kupiga vita uvuvi huo kwa sababu rasilimali za ziwa hilo zinazidi kupungua.
“Rasilimali za Ziwa Victoria zinapungua,hilo halina mjadala.Takwimu zitatusaidia ili wanaofanya uvuvi haramu na wanaowasaidia waone umuhimu na hakuna haja ya kupiga kelele,mwaka 2023/24 mchango wa uvuvi ulikuwa asilimia 67,unagusa asilimia kubwa na inatubidi kukilinda chanzo hiki,hivyo sekta ya uvuvi haitakuwa na mzaha,”amesema.
Amesema takwimu zinaonesha mwaka 2019 uvunaji wa sangara ulikuwa ni tani 91,709 lakini mwaka 2023 umeshuka hadi tani 85,265 huku uvunaji wa dagaa mwaka 2019 ukiwa ni tani 122,000 ambapo uvunaji umezidi kuongezeka.
“Mwaka 2023/24 ili kwenda kidijitali tunafanya doria zaidi na tunategemea kuweka mfumo wa ufuatiliaji vyombo vya uvuvi,ili kuwabaini wanaofanya uvuvi haramu,zitanunuliwa ndege nyuki (drones) za kuwasaka wavuvi haramu zenye uwezo wa kutembea kilometa 150,”amesema Profesa Sheikh.
More Stories
TAKUKURU,rafiki yanufaisha wananchi Mwanza
Mhandisi Samamba awasisitiza maafisa madini kusimamia usalama wa migoni msimu wa mvua
Wapinzani kutimkia CCM ishara ya ushindi Uchaguzi Serikali za Mitaa