Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online – Geita
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko, ametembelea banda la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwenye Maonyesho ya Teknolojia ya Madini yanayohitimishwa leo Septemba 28,2025 mkoani Geita ambapi amepata maelezo ya kina kuhusu namna BoT inavyoshirikiana na wachimbaji wa madini, ili kuwaunganisha na mifumo rasmi ya kifedha kwa maendeleo yao binafsi na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza mbele ya Dkt.Biteko wakati wa ziara hiyo, Meneja wa Uhusiano wa Umma na Itifaki wa Benki Kuu ya Tanzania, Vicky Msina amesema BoT imeweka mazingira rafiki kwa wachimbaji wadogo na wa kati kujiunganisha moja kwa moja na benki kuu kwa ajili ya kuuza dhahabu wanazozalisha.
Amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha akiba ya fedha za kigeni ya Taifa.
“Sasa hivi tupo hapa kwa ajili ya kuelimisha wananchi na wachimbaji kuhusu masuala mbalimbali ya kifedha ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika mfuko wa Serikali .”amesema
Aidha, BoT inawahamasisha wachimbaji hao kuwekeza kwenye dhamana za serikali, ikisisitiza kuwa kundi hili lina uwezo mkubwa wa kifedha unaoweza kusaidia kuendesha miradi ya maendeleo nchini, na wakati huo huo, likijiimarisha kiuchumi.
“Tunawasihi hawa wenzetu wa sekta ya madini waje kuwekeza kwenye dhamana za serikali,tunafahamu kwamba wanakusanya fedha nyingi, na wakizielekeza katika uwekezaji huu, serikali itaweza kuendesha miradi ya maendeleo na wao pia watanufaika,” ameongeza.
Mbali na uwekezaji amesema BoT pia inatoa elimu kwa wachimbaji kuhusu matumizi sahihi ya mifumo ya kifedha, hasa malipo kupitia mifumo rasmi inayosimamiwa na benki kuu elimu itakayowasaidia wachimbaji kuelewa umuhimu wa kupanga matumizi ya fedha kwa malengo ya maendeleo.
“Tunawaeleza kuwa unapokopa, hakikisha unakopa kwa malengo. Siyo kukopa halafu unanunua viti au vitu visivyo na tija. Tunawapa mwongozo juu ya namna bora ya kutumia mikopo ili kuongeza thamani katika maisha yao,” alifafanua.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina