


Na Joyce Kasiki, Timesmajira online,Tanga
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imewahimiza wananchi kuhakikisha wanachagua na kutumia huduma za taasisi za fedha zilizosajiliwa rasmi na benki hiyo ili kujilinda dhidi ya hatari za kifedha na kuchangia ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewaleo Januari 21,2026 na Afisa Mkuu Mwandamizi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Mwile Kauzeni, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Kifedha yanayoendelea kitaifa mkoani Tanga.
Kauzeni amesema kuwa wananchi wanaotaka kupata mikopo kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao za kiuchumi wanapaswa kwanza kuzitambua taasisi za fedha zilizosajiliwa na Benki Kuu ya Tanzania kwa kutembelea tovuti rasmi ya BoT ya www.bot.go.tz, ambako kuna orodha ya benki, taasisi nyingine za fedha pamoja na maduka ya kubadilisha fedha za kigeni (bureau de change).
Amefafanua kuwa mwananchi anatakiwa kuwa makini katika kuchagua taasisi ya kifedha inayomfaa, ikiwemo kufahamu aina ya mikopo inayotolewa na taasisi husika kabla ya kuingia makubaliano ya mkopo.
“Ni muhimu kwa mkopaji kujaza fomu, kuelewa masharti ya mkopo, kutambua wajibu wake wa kufanya marejesho kwa wakati, huku taasisi ya fedha nayo ikifahamu wajibu wake kwa mteja,” amesema Kauzeni.
Aidha, amewahimiza wananchi, hususan wanawake, kuhakikisha wanakopa kwenye taasisi zilizosajiliwa ili kuepuka mikopo hatarishi kutoka kwa taasisi zisizo halali.
Katika maelezo yake, Kauzeni amesema BoT ina jukumu la kusimamia benki, taasisi za fedha, maduka ya kubadilisha fedha za kigeni pamoja na taasisi nyingine kama benki za maendeleo na taasisi za fedha zinazotoa mikopo kwa njia ya vifaa.
Amesisitiza kuwa taasisi zote lazima zipate leseni kutoka BoT kabla ya kuanza kutoa huduma na zinapaswa kuzingatia sheria na kanuni za usimamizi wa sekta ya fedha.
Kwa upande wake, Afisa Sheria Mwandamizi kutoka Kurugenzi ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Kifedha, Kitengo cha Malalamiko ya Wateja wa Huduma za Kibenki, Ramadhani Miyonga, alisema BoT imeweka mabanda maalumu katika maonyesho hayo kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kushughulikia malalamiko yao dhidi ya taasisi za fedha zilizosajiliwa.
Miyonga ameeleza kuwa BoT imeanzisha mfumo wa kidigitali uitwao “Sema na BoT”, unaopatikana kupitia tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania ambapo wananchi wanaweza kuwasilisha malalamiko yao.
Ameongeza kuwa BoT pia imetoa namba ya bure 0800 111 100 kwa wananchi wanaohitaji msaada au maelekezo ya namna ya kutumia mfumo wa Sema na BoT.
Hata hivyo, Miyonga amesisitiza kuwa msaada huo unahusu wateja wa taasisi za fedha zilizosajiliwa pekee, akiwataka wananchi kuepuka kushirikiana na taasisi zisizosajiliwa kwani BoT haiwezi kuzisaidia endapo kutatokea migogoro.
Amefafanua kuwa kwa mujibu wa kanuni za malalamiko ya wateja wa huduma za fedha za mwaka 2019 zilizofanyiwa marekebisho mwaka 2025, mteja mwenye malalamiko anatakiwa kwanza kuwasilisha malalamiko yake katika taasisi ya fedha husika, ambayo inapewa muda wa siku 14 kuyashughulikia.
“Endapo mteja hataridhika na majibu au hatapata majibu ndani ya muda huo, ndipo anapopaswa kuwasilisha malalamiko yake kupitia mfumo wa SEMA na BoT,” amesema Miyonga.
BoT imewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika maonyesho ya Wiki ya Huduma za Kifedha ili kujifunza masuala mbalimbali ya kifedha yatakayowawezesha kufanya maamuzi sahihi na kuchangia katika ujenzi wa uchumi wa taifa.
Mapema akizungumza mbele ya Naibu Waziri wa Fedha Laurent Luswetula alipopita kwenye Banda la BoT,Meneja wa Mawasiliano Benki Kuu ya Tanzania
Vick Msina amesema kwenye maonyesho hayo wanatoa Elimu ya fedha kwa wananchi na majukumu ya benki Kuu kwa ujumla.
Pia wanawaelekeza wastaafu wanaopita kwenye Banda hilo,wanawaelekeza namna wanavyoweza kuwekeza kupitia shughuli nyingine ikiwemo kuwekeza kwenye dhamana za Serikali kwa.manufaa yao na uchumi wa Taifa.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama