March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

‎BoT yaagizwa kuimarisha udhibiti wa sekta ya fedha kulinda wananchi dhidi ya madhara ya mikopo umiza





‎Na Joyce Kasiki, Timesmajira online,Tanga

‎NAIBU Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula, ameziagiza mamlaka husika zikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuimarisha udhibiti wa sekta ya fedha ili kuwalinda wananchi dhidi ya madhara ya mikopo umiza inayotolewa na taasisi zisizo rasmi, maarufu kama “mikopo kausha damu”.

‎Luswetula alitoa agizo hilo wakati wa uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa, yanayofanyika mkoani Tanga.

‎Alisema kuwa kuimarishwa kwa udhibiti kutasaidia kuzibaini taasisi au watu binafsi wanaotoa mikopo hiyo kandamizi, hatua itakayowezesha kuchukuliwa kwa hatua za kisheria dhidi yao na kuwaepusha wananchi na hasara ikiwemo kupoteza mali na vitu vyao vya thamani.

‎Aidha, aliwaonya watoa huduma za fedha wanaofanya shughuli zao bila kufuata taratibu, ikiwemo kutosajiliwa na mamlaka husika kama Benki Kuu ya Tanzania na taasisi nyingine zilizopewa dhamana ya kusimamia sekta ya fedha, kuacha mara moja tabia hiyo.

‎Kwa upande wa wananchi, Naibu Waziri aliwahimiza kuhakikisha wanapata taarifa sahihi kuhusu uhalali wa taasisi wanazokusudia kukopa, pamoja na kusoma na kuelewa kwa kina mikataba ya mikopo kabla ya kuisaini, ili kujiepusha na hasara ambazo wengi wamezipata kutokana na kukubali masharti yasiyoeleweka.

‎Akizungumza kuhusu maendeleo ya sekta ya fedha, Luswetula alisema kumekuwepo na mafanikio makubwa kufuatia maboresho yaliyofanyika, hata hivyo bado kuna changamoto ya uelewa mdogo wa masuala ya fedha kwa wananchi, ikiwemo uandishi wa maandiko ya miradi na matumizi ya huduma zisizo rasmi.

‎“Ni matarajio yangu wananchi watajitokeza kwa wingi katika viwanja vya Usagara jijini Tanga kwa kipindi chote cha Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa, ili kupata elimu ya fedha na kutumia huduma sahihi kama kufungua akaunti, kuweka akiba, kukata bima, kuwekeza pamoja na kuwasilisha malalamiko na maoni yao kuhusu sekta ya fedha,” alisema Luswetula.

‎Pia alitoa wito kwa waelimishaji wa masuala ya fedha katika ngazi zote kuhakikisha wanatoa elimu hiyo kwa weledi, kwa lugha rahisi inayoeleweka, huku wakizingatia maoni na ushauri wa wananchi kwa lengo la kuboresha sera, bidhaa na huduma za kifedha nchini.