December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Boost ilivyoboresha miundombinu ya elimu Ilemela 

Judith Ferdinand 

Licha ya  changamoto mbalimbali zinazo ikabili sekta ya elimu nchini, Serikali pamoja na wadau,wamekuwa wakifanya jitihada mbalimbali za kuboresha sekta hiyo ikiwemo  kuanzisha mradi wa Boost,wenye lengo la kusukuma maendeleo ya elimu msingi nchini kwa shule za awali na msingi.

Oktoba 15,2023 Rais Samia Suluhu Hassan alizindua shule za msingi zilizojengwa na Mradi wa kuimarisha Shule za Awali na Msingi (BOOST) katika shule ya msingi Imbele  Manispaa ya Singida.

Uzinduzi huo ulifanywa kama alama ya kuzinduliwa kwa shule zote nchini zilizojengwa kupitia mradi huo ambao unasaidia watoto kupata elimu bora.

BOOST ni mradi unaotekelezwa kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2021/2022, kupitia Wizara za Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais-TAMISEMI chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia. unataraji kugharimu shillingi tirioni 1.5.

Taarifa za serikali zinaonesha kuwa hadi Septemba 2023 Sh. Bilioni 230 zilikuwa zimeishatolewa huku ujenzi wa shule za msingi 194, madarasa ya awali 364 na , madarasa ya shule za msingi 2,303 ukiwa umekamilika.

Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ni moja ya wanaufaika wa mradi wa Boost,ambayo  ina Kata 19,shule za msingi 152, kati ya hizo za serikali ni 83, binafsi 69.Wanafunzi wa shule za serikali msingi ni 99,343, kati yao wavulana 44,505 na wasichana 45,837.

Majira inabisha hodi Kata ya Kahama mtaa wa Buteja, Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela na kutembelea shule mpya ya msingi Buteja,na kuzungumza na wanafunzi,walimu na wananchi.

Je?, changamoto zipi ziliwakabili wanafunzi katika harakati za kusaka elimu kabla ya ujenzi wa shule   hiyo,unanga na Mwandishi wa Makala haya ili kufahamu yote.

Changamoto kabla ya ujenzi wa shule ya msingi Buteja 

Bryson Obed,mwanafunzi wa  darasa la sita shule ya msingi Buteja,awali alikuwa anasoma shule ya msingi Kahama iliopo Kata ya Kahama, anaishi mtaa wa Kadinda,anaeleza kabla ya kuhamishiwa katika shule hiyo mpya,walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya wanafunzi kuwa wengi huku madawati yakiwa hayawatoshi,hali iliowalazimu kukaa chini.

Prisca Bernard,aliyekuwa anasoma shule ya msingi Lukobe,kabla ya kuhamishiwa shule mpya ya Buteja,anaeleza kuwa, katika shule hiyo walikuwa wanatumia muda mrefu kutoka nyumbani kwenda shuleni akitolea mfano kuwa wakitoka nyumbani saa 1 kamili asubuhi anafika shuleni saa moja na dakika 45,hali ilikuwa inachochea    kutokufanya vizuri  katika masomo kwa sababu walikuwa wanapitwa na baadhi ya vipindi.

Agnes John awali aliyekuwa anasoma shule ya msingi Buswelu,anasema wakikabiliwa na changamoto ya upungufu wa madawati hali iliowalazimu kukaa wanafunzi watano kwenye dawati moja na wakati mwingine chini.Pia wanafunzi walikuwa wengi huku vitendea kazi vikiwa vichache ikiwemo  vitabu.

Mmoja wa wananchi wa mtaa wa Buteja Kata ya Kahama,Rebecca Elinzu,anasema kabla ya mradi huo watoto wao walikuwa wanahangaika kufuata huduma ya elimu mpaka shule ya msingi Lukobe,iliopo mbali na wanapoishi.

“Changamoto zilikuwa nyingi,barabara zilikuwa hazipitiki hasa wakati wa masika hivyo kusababisha watoto kutohudhuria masomo.Pia magari yalikuwa mengi na hatari kwa watoto hasa wa elimu ya awali(chekechea),hivyo tulipata shida kuwapeleka na kuwafuata shuleni,hali iliotupunguzia muda wa kufanya shughuli za kiuchumi na za  nyumbani,”.

Mradi wa Boost Halmashauri ya  Ilemela 

Mratibu wa Boost Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Ofisa Elimu Vifaa na Takwimu,Johannes John,anasema,”Utekelezaji wa majukumu yetu katika  elimu ya awali na msingi,kuna vitu ambavyo vinakwamisha elimu isiwe sawa,hivyo baada ya kuona changamoto hizo.Serikali ikatafuta fedha kwa ajili ya kuendesha mradi wa Boost,ambao utapunguza changamoto zinazohusiana na elimu ya awali na msingi,”.

John anasema,awamu ya kwanza ya utekelezaji  wa mradi huo wa Boost,Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,kwa mwaka 2022/2023 ilipokea fedha kiasi cha zaidi ya bilioni 1.5 ,zilihusika katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo ujenzi wa shule mbili mpya za msingi zenye mikondo miwili,Kata ya Buswelu shule inaitwa Busenga na Kata ya Kahama shule inaitwa Buteja.

Ujenzi wa shule mpya za msingi

John anaeleza kuwa kati ya fedha kiasi cha zaidi ya  bilioni 1.5,zilizotolewa kutembelea mradi huo,ujenzi wa shule zote mbili za Busenga na Buteja,walipata bilioni 1.086 ambapo  kwa kila shule walipata kiasi cha milioni 543.

Hata hivyo Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule ya msingi Buteja,Mary Mushi,anasema shule hiyo iliojengwa jumla ya madarasa 16, kati ya hayo,14 shule ya msingi na elimu awali mawili.Ina eanafunzi 831, kati yao wavulana 397 na wasichana 434, mahitaji ya walimu ni 18,waliopo 13 kati yao wakike 9 na wakiume 4, upungufu ni walimu 5. 

Pia miundombinu ya vyoo inakidhi mahitaji ya wanafunzi wote wakiwemo wenye mahitaji maalum,ambapo shule ina matundu ya vyoo 21 kati ya hivyo,13 kwa elimu msingi huku wasichana 8 na wavulana 5.

Elimu awali matundu ya vyoo 6,kati ya hivyo vitatu wasichana na vitatu wavulana,huku matundu mawili ya vyoo kwa ajili ya walimu kati ya hayo moja wanaume na moja wanawake.

Darasa moja wanafunzi takribani 80, yenye madawati 25, hivyo kwenye dawati moja wanakata wanafunzi watatu. Hivyo shule nzima madawati yapo takribani 350.

Maboresho ya miundombinu  shuleni

Mratibu wa mradi wa Boost Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Johannes John, anasema utekelezaji mwingine uliofanyika kupitia fedha hizo ni ujenzi wa vyumba 16 kwa shule nne za msingi, ambao umegharimu kiasi cha milioni 400 huku kila shule ikipata milioni 100 kwa ajili ya kujenga  vyumba vinne vya madarasa.Ambapo shule hizo ni Igombe Kata ya Bugogwa,Nyamadoke na Nyamh’ongolo(Kata ya Nyamh’ongolo) pamoja na Nyamilorerwa Kata ya Shibula.

“Kiasi cha milioni 25.2, zilitumika kujenga matundu  12 ya  vyoo,katika shule nne za msingi ikiwemo Igombe  iliopo Kata ya Bugogwa,Nyamadoke na Nyamh’ongolo(Kata ya Nyamh’ongolo) pamoja na Nyamilorerwa Kata ya Shibula.Ambapo Kwa kila shule ilipata kiasi cha milioni 6.3 kwa matundu matatu ya vyoo na kila tundu liligharimu kiasi cha milioni 2.1,”.

Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Buteja iliojengwa kwa mradi wa Boost wakiwa darasani

Ujenzi wa vyumba vya madarasa vya mfano elimu ya awali

John anasema,walijenga vyumba viwili vya madarasa ya mfano elimu ya awali  katika shule ya msingi Chasubi iliopo Kata ya Kayenze,vyoo na bembea,ambapo ujenzi uliogharimu kiasi cha milioni 66.1.

“Utekelezaji wa mradi wa boost kwa mwaka 2022/2023 Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela tulipokea kiasi cha bilioni 1 milioni mitano sabini na nne na  laki tisa,na miundombinu imekamilka na imeanza kutumika ambapo wanafunzi tayari wapo shuleni kwa shule zote mbili wakiendelea na masomo,”.

Sanjari na hayo anasema,awamu nyingine ya mwaka 2023/2024, Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,ilipokea kiasi cha milioni 510.Kati ya fedha hizo,milioni 351.5, kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya msingi Masemele  yenye mkondo  mmoja iliopo Kata ya Shibula.

Huku milioni 155.5 kwa ajili ya shule ya msingi Kayenze Ndogo,iliopo Kata ya Bugogwa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili ya mfano ya elimu ya awali,matundu 12 ya vyoo na vyumba vitatu vya madarasa.Huku kiasi cha milioni 3,ni  kwa ajili ya ufuatiliaji wa miradi.Ambapo kwenye shule husika wapo katika hatua  za awali  kwa ajili ya ujenzi.

Changamoto walizokutana nazo katika kutekeleza mradi wa Boost 

John,anasema walikutana na  changamoto ndogo wakati wa utekelezaji  wa mradi,ambazo waliweza kuzitatua na kufanikisha kukamilisha kwa haraka mradi huo,kwani baada ya wananchi kutafuta maeneo ya kujenga shule hizo ilikuwa rahisi kwao kutekeleza.

Faida ya mradi wa boost 

Mratibu huyo wa mradi wa Boost Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Johannes John,anasema,Wilaya ya Ilemela ilikuwa na watoto wanaoishi mbali na shule,hivyo ilikuwa  shida kutembea kwenda na kurudi shuleni.

“Baada ya uenzi wa shule hizi mpya mbili, wamekuwa karibu na shule,umepunguza utoro kwa wanafunzi,umerahisisha ufundishaji,kwa sababu ya wingi wa vyumba vya madarasa umesaidia kuondoa msongamano,”anaeleza John na kuongeza:

“Wanafunzi wanafanya vizuri,japo hatujafikia asilimia 100,kwani ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba umeongezeka,wakati mradi unaanza mwaka 2022 ufaulu kwa Halmashauri yetu ya Ilemela ulikuwa kwa asilimia 95 na mwaka 2023 ufaulu ulikuwa asilimia 95.639, hivyo boost imetuondoa katika hali fulani,” anaeleza John na kuongeza:

“Umesaidia watoto kukaa kwenye madawati na kuondokana na adha ya kukaa chini kutokana na uhaba wa madawati.Madarasa 40,kila darasa madawati 25.Hivyo kupitia mradi huu wa Boost yamepatikana madawati 1000 kwa shule za msingi.Huku shule za awali kila darasa viti 30,hivyo jumla viti 60,”.

“Mradi huo umeboresha rasilimali mpya na kuboresha zilizopo mfano shule ilikuwa na madarasa 30 lakini wameongezea manne,kulikuwa na matundu ya vyoo manne tumeongezea matatu maana yake tumeboresha,”.

Madarasa mawili ya mfano elimu ya awali katika shule ya msingi Buteja yaliojengwa kupitia mradi wa Boost

Aidha anaeleza kuwa Boost  inasimamia uandikishaji wa elimu ya awali, wamepata mafanikio ambapo mwaka 2022waliandikisha wanafunzi  3813 sawa na asilimia 72 huku mwaka 2023 uandikishaji ulikuwa 5563, sawa ana asilimia 102.

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule ya msingi Buteja,Mary Mushi, anasema kupitia mradi huo mazingira yameboreshwa,hivyo kuwavutia wanafunzi kuja shule na kusaidia suala la utoro kupunguza kwani ulikuwepo kwa asilimia 30 lakini sasa upo kwa asilimia 5.

“Baada ya mradi wa boost hali ya ufaulu imekuwa nzuri na umeongezeka,mfano darasa la saba mwaka huu,ilikuwa ya kwanza katika mtihani wa Moko(mock) Wilaya kwa shule za Serikali,”.

Mmoja wa wananchi wa mtaa wa Buteja Kata ya Kahama, Rebecca Elinzu,anasema wamefurahi,watoto wao  wamesogezewa shule karibu,hali iliosaidia kupunguza utoro kwa wanafunzi ambao wengi wao walikuwa wanaishia njiani.

“Mradi huu ulivyokuja utoro kwa wanafunzi umepungua,maana wengine walikuwa wanasingizia kuwa wamefika shule kumbe hajafika na ilikuwa ngumu kwa mzazi kuweza kumfatilia kwa sababu ilikuwa mbali, hapa ni rahisi mzazi kujua kama mtoto hajafika shule na kuchukua hatua.Wananchi wenzangu waweze tufuatilia maendeleo ya watoto wao shuleni kwa kushirikiana na walimu,kwani elimu ni muhimu zamani tulikuwa tunasoma tunaishia darasa la Saba na wengine ata lasaba walikuwa hawafiki,lakini Leo hii tumeona elimu imekuwa kama kipato cha mwanadamu.

“Ninegundua watu wengi hata watoto,wanapenda vitu kizuri.Baada ya kujenga shule hii ya msingi ya  mfano Buteja,watoto wamekuwa wanahudhuria shuleni,wazazi wanazingatia elimu ya watoto wao kwa sasa,maana zamani nilikuwa naambiwa utoro,lakini sasa sijapata malalamiko ya utoro,”anaeleza Mwenyekiti wa Mtaa wa Buteja Mabele Elias.

“Tunafurahia,Rais Samia kutujengea shule hii mpya ya Buteja,ambayo imetupunguzia umbali wa kutembea na kufika shule kwa dakika chache,tunajisomea na tunaendelea vizuri na masomo,hivyo tunatarajia kufaulu,”anaeleza Bryson Obed mwanafunzi wa darasa la sita shule ya msingi Buteja.

Philipo Malilemba, mwanafunzi wa darasa la sita shule ya msingi Buteja,anasema,”Madawati yapo ya kutosha hivyo hatukai chini,walimu wanafundisha vyema.Namuahidi Rais.Samia,wazazi na walimu,mwakani tunapoingia darasa la Saba tutafanya vizuri, hatutaiangusha shule yetu,hivyo tutafaulu ili kuendelea na elimu ya sekondari hadi chuo na kuweza kutimiza ndoto zangu za kuwa mwanasayansi mkubwa,”.

Agnes John awali alikuwa anasoma shule ya msingi Buswelu, anasema kuwa,”Tumepata mabadiliko kwa sababu shule niliotoka madarasa yalikuwa machache na wanafunzi walikuwa wengi.Tulipofika hapa  Buteja tumeona mabadiliko kwani vitendea kazi vipo kama madarasa,madawati na vitabu,”.

Ushirikishwaji wa wananchi katika mradi wa Boost 

Mwenyekiti wa Mtaa wa Buteja Kata ya Kahama,Mabele Elias,anaeleza kuwa kabla ya mradi kuanza walishirikishwa wananchi ili waweze kubainisha eneo ambalo litajengwa shule ya msingi ya mfano ambalo hakuna fidia ,bahati iliangukia mtaa wa Buteja.

“Wananchi walishiriki  katika ujenzi wa shule hiyo,ikiwemo kufanya usafi kwa kufyeka majani,kusawazisha na kuondoa taka.Pia  nilihamasisha wananachi kufanya kazi  ndogo ndogo ambazo hazihitaji utaalamu  na siku ya ufunguzi wa shule hiyo wananchi  pia walishiriki,”.

Maboresho gani yanatakiwa

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule ya msingi Buteja,Mary Mushi, anasema ili shule hiyo iendelee kuwa bora na kumvutia,wanahitaji kuwekewa  uzio,vifaa vya kufundisha vya  kisasa,mfano kompyuta(computer),chumba cha maktaba kwa ajili ya wanafunzi kujisomea ili kuchochea zaidi ufaulu pamoja na maabara ambayo itatumika kuwajenga kwa vitendo wanafunzi wanapenda sayansi wakiwa bado wadogo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Buteja,Mabele Elias,anasema licha ya mradi huo kuwa mzuri,ameiomba Serikali na wadau waweze kuweka uzio ili kuimarisha ulinzi na usalama wa wanafunzi,”Shule  ni nzuri,ila kuna watu wana mitazamo yao,wanaingia wanavunja vioo,taa,kwaio sasa tukitengeneza uzio tutakuwa tumeboresha shule yetu na kuwa na ulinzi,”.

Muonekano wa choo cha wanafunzi wa elimu ya awali katika shule ya msingi Buteja

Nini mkakati wa Serikali 

Mratibu wa mradi huo wa Boost Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, John,anasema,mkakati ni kuhakikisha jamii inashiriki kikamilifu  afua zote za mradi wa Boost,hasa  zile ambazo hazihitaji fedha.Pia kuwa na usimamizi thabiti  kutoka kwa  Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri na wengine.

Huku walengwa wa mradi huu ni wanafunzi,walimu,jamii husika,ambapo watoto wakipata elimu ni manufaa kwao pia na wadau wa elimu kwa ujumla.Ni endelevu na wataendelea  kuibua mahali penye changamoto.

“Mradi huu umeondoa changamoto ya mrundikano wa wanafunzi Kata ya Kahama na Buswelu.Shule hii imepunguza mwendo kwa wanafunzi kufuata huduma ya elimu, ambapo kwa sasa inahudumia watoto kutoka mitaa ya Buteja,Kadinda,Kigala na Majengo Mapya, wilayani Ilemela,”.

Muonekano wa choo cha wàlimj wa shule ya msingi Buteja iliojengwa kupitia mradi wa Boost
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Buteja wakiwa darasani