January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bongo Movie wampongeza Rais Dkt. Samia safari ya Korea

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar

WASANII wa Filamu na Tamthilia nchini Tanzania wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kugharamia safari yao ya nchini Korea kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu sekta ya sanaaa ya filamu ya tamthilia duniani.

Wasanii hao walizungumza na waandishi wa habari jana mchana, jijini Dar es Salaam, baada ya kurejea kutoka Korea walipokwenda tangu Julai 1, mwaka huu wakijifunza namna ya kufanya kazi zao za kisanii kama njia ya kujiletea maendeleo na kukuza sekta hiyo nchini Tanzania.

Baadhi ya wasanii waliokwenda Korea ambao wametoka mbele ya waandishi wa habari kumshukuru Dkt. Rais Samia ni pamoja na Steve Nyerere kama Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti Idris Sultan, Wema Sepetu, Irene Uwoya, Monalisa Cherly, Irene Paul, Gertrude Mwita, Godliver Gordian nk.

Wasanii hao kwa umoja wao wamempongeza Dkt Samia kwa kitendo chake cha kugharamia safari yao ya Korea. Wamesema ni wakati sasa wa kufanyia kazi elimu waliyoipata wakiwa nchini Korea, wakiamini watafikia hatua nzuri.

Kwa upande wa maboresho ya sekta hiyo, wasanii hao waliitaka Serikali kuweka mikakati zaidi kugharamia utendaji kazi wa Sanaa wa Tanzania kama walivyofanya Korea kwa kuweka bajeti ya uandaaji wa filamu zao hali iliyoibua na kuendeleza sekta hiyo.

Safari ya wasanii hao imekuja wakati ambao Rais Samia alitangaza neema kubwa kwa wasanii ya kugharamia safari zao pindi atakapokuwa na ziara za kikazi nje ya nchi.