December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bondia Hassan Mwakinyo. (Picha na Mtandao).

Bondia Mwakinyo,Kayemba kuzichapa Agosti 14

Na Penina Malundo,TimesMajira Online

BONDIA Mtanzania Hassan Mwakinyo anatarajia kupanda ulingoni Agosti 14, mwaka huu kumenyana na bondia kutoka Congo, Tshibangu Kayembe.

Pambano hilo la aina yake la kuwania ubingwa wa WBF linatarajiwa kufanyika katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam ambapo mabondia hao watapambana raundi 12.

Akizungunzia mtanange huo, Mwakinyo amesema, yuko tayari kwa pambano hilo, kwani amejiandaa vya kutosha kuhakikisha anamaliza pambano hilo mapema.

Amesema, maandalizi mazuri ambayo ameyafanya na kuendelea kuyafanya yanazidi kumpa morali zaidi kuelekea pambano hilo ambalo hatokubali kuiangusha nchi.

“Tarehe 14 mwezi ujao natamani sana pambano lifike hata siku zikimbie tano tano, nimejiandaa na naendelea kujiandaa sina shaka wala hofu na bondia yoyote yule aje tu tukutane ulingoni.

“Namuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kuunga mkono jitihada za mabondia hapa nchini kama ambavyo amefanya mambo makubwa katika kuendeleza nchi na jina lake kuzidi kuwa kubwa,”amesema.

Anasema, Rais akisapoti mchezo huo hata wao mabondia itakuwa vyema kwao na itazidi kuwapa morali ya hali ya juu kuzidi kulitangaza Taifa.

“Naimani kubwa na Rais wetu pia nawaomba wadhamini nao wasiutupe mchezo wetu huu unapeperusha vyema bendera ya Tanzania kupitia sisi na hiyo Agosti 14 nitawahahakikishia Watanzania mimi ni nani,”amesema.

Kwa upande wake Mratibu wa matukio kuelekea pambano hilo, Beautrice Said amesema, katika pambano hilo kutakuwa na mapambano ya utangulizi nane ya utangulizi ambayo yatawakutanisha mabondia wa hapa Tanzania.

Baadhi ya mapambano hayo ni Seleman Kidunda ambaye ataumana na Shaban Kaoneka uzito kg 72, Issa Nampepecha na Khareed Manjee kg 61.

Pia katika pambano hilo kutakuwa na pambano lingine la Kimataifa ambalo litamkutanisha Tony Rashid atakayemualika Mkenya Gabriel Ochieng pambano la raundi 12 kutetea ubingwa wa ABU.

Mwakinyo amepambana mapambano 18 na kupoteza mawili huku mpinzani wake Kayembe amecheza mapambano 12 kashinda 9 na kutoka sare 3.