Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Tanga
RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati anahutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili 22, 2021, alijipambanua kwa kuhakikisha anamtua ndoo kichwani mwanamke wa Kitanzania kwa huduma hiyo kuwa karibu na wananchi na ikipatikana mijini na vijijini.
Na katika kuweka msisitizo, katikati ya hotuba yake bungeni, alimuamsha Waziri wa Maji Jumaa Awezo kwa kumueleza amemkabidhi wizara hiyo kwa matumaini kuwa atafikia malengo na matumaini ya Rais Dkt. Samia ya kuisaidia Sekta ya Maji kuondoa kero ya muda mrefu upatikaaji wa maji mijini na vijijini.
Matamanio ya Rais Dkt. Samia yalikwenda sambamba na kutoa fedha nyingi kwenye Sekta ya Maji, ambapo kupitia Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), na mamlaka za maji mijini wameonesha kufanya kazi kubwa za kujenga miundombinu ya miradi ya maji kupitia maji ya mtiririko na ya visima (kuvuta kwa pampu) kutoka kwenye vyanzo mbalimbali.
Lakini pamoja na jitihada hizo, bado ilionekana kuna maeneo mengi ambayo hayana vyanzo vya maji ya mtiririko, lakini kama maji hayo yatatafutwa chini ya ardhi bado inaweza kuwa msaada mkubwa kwa wananchi wanaoishi maeneo makame ambayo hayana vyanzo vya maji ya mtiririko kabisa.
Katika kutimiza azma yake, Rais Dkt. Samia alinunua magari ya kuchimba visima na kupata maji chini ya ardhi, na kila mkoa ulipata gari moja. Na ununuzi wa magari hayo ulikwenda sambamba na kutafuta maji chini ya ardhi kwa nguvu zote.
Na hiyo ni baada ya wabunge kutoa kilio kwa Serikali kuwa, pamoja na jitihada za Serikali kujenga miradi mingi nchini, lakini bado wananchi hasa wa vijijini, wanatafuta maji kwa umbali mrefu, huku, na hasa wanawake wakihatarisha maisha yao na ndoa zao kwa ajili ya kutoka usiku wa manane kutafuta maji.
Ndipo Rais Dkt. Samia alipokuja na mpango wa kuchimba visima 900 kwenye majimbo 180 nchini ili kuona wanapunguza kama sio kuondoa kabisa tatizo la maji, na hasa vijijini.
Na ili kupata maji hayo, ni lazima wataalamu waweze kufanya usanifu wa wapi maji hayo kuna uwezekano wa kupatikana, na kazi hiyo ya kufanya utafiti wamekabidhiwa Mabonde tisa nchini ya kutafuta maji hayo.
Mwandishi wa makala haya amefanya mahojiano maalumu na Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Pangani (PBWB) Mhandisi Segule Segule yalipo Makao Makuu ya Bonde hilo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
Mhandisi Segule alisema kama ilivyo mabonde mengine, Bonde la Maji la Pangani wamepewa kazi ya kutafiti upatikanaji maji chini ya ardhi kwenye mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha, ambapo jumla ya maeneo 117 yamefanyiwa utafiti huo kwenye majimbo mbalimbali yaliyopo kwenye mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga, na kati ya maeneo hayo, 58 yamependekezwa kwa ajili ya uchimbaji.
***BONDE LA PANGANI
Bodi ya Bonde la Pangani iliyopo chini ya Wizara ya Maji, ni moja ya mabonde tisa yaliyopo nchini. Na moja ya kazi yake kubwa ni kwa ajili ya kusimamia matumizi endelevu ya rasilimaji maji, ambapo maji yana kazi kubwa mbili. Moja kuyasimamia ili yaendelee kuwepo, na mbili ni Serikali kuyajengea miundombinu na kuyasambaza ili yaweze kuwafikia wananchi.
“Bodi za mabonde ya maji zimewekwa kwa ajili ya kusimamia matumizi endelevu ya rasilimaji maji. Kama mnavyojua, nchi yetu ina rasilimali nyingi kama misitu, ardhi na madini. Na maji vivyo hivyo, ni sehemu ya rasilimali.
Lakini kwenye maji wanatujua kwa ajili ya usambazaji maji, lakini kwenye maji tuna kazi kubwa mbili, moja kuyasimamia ili yaendelee kuwepo, na mbili ni Serikali kuyajengea miundombinu na kuyasambaza ili yaweze kuwafikia wananchi” anasema Mhandisi Segule.
Mhandisi Segule anasema katika kuona maji hayo yanakuwa endelevu ili wananchi na wadau wengine ambao ni watumia maji waweze kunufaika na upatikanaji wa maji hayo, Serikali kupitia Wizara ya Maji iliunda taasisi za usimamizi wa maji, ambapo kwa mijini kuliundwa Mamlaka za Maji, na vijijini kuliundwa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).
Lakini kwa vile maji hayatumiki kwa ajili ya kunywa tu, bali kuna watumiaji wengine wakubwa wa maji kama kilimo cha umwagiliaji ambao wanachukua asilimia 80 ya maji yote, huku kukiwa na mifugo, na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), ambao hao wote wanatumia maji, ndipo Serikali ikaunda taasisi ya mabonde ya maji nchini ili waweze kuratibu watumiaji wa maji wote nchini.
“Sasa katika Wizara ya Maji, wenye kazi ya kusambaza maji hayo ni Mamlaka za Maji mijini, na RUWASA kwa upande wa vijijini. Lakini kwa vile maji hayatumiki kwa ajili ya kunywa tu, bali kuna watumiaji wengine wakubwa wa maji kama kilimo cha umwagiliaji ambao wanachukua asilimia 80 ya maji yote, huku kukiwa na mifugo, na TANESCO), ambao hao wote wanatumia maji, ndipo Serikali ikaunda taasisi ya mabonde ya maji nchini ili waweze kuratibu watumiaji wa maji wote nchini.
“Kwa hiyo sisi bodi za maji za mabonde kazi yetu ni kuwaratibu watu wote watumiaji wa maji. TANESCO naye anatumia maji ili kuzalisha umeme, je, tumuache ajiratibu mwenyewe!… hilo haliwezekani. Kwa hiyo Serikali iliona umuhimu wa mabonde tangu enzi za Mwalimu Julius Nyerere (Rais wa Awamu ya Kwanza wa Tanzania). Kwenye ile Sheria yetu ya mwaka 1974, tulikuwa tunasimamia maji chini ya mikoa ambapo chini yake kulikuwa na wataalamu na watendaji wote wanaoshughulikia maji kwa kufuata mkoa kama rasilimali” anasema Mhandisi Segule.
Segule anasema, lakini jambo hilo lilikuwa gumu sababu vyanzo vya maji vinavyolisha mkoa mmoja vinaweza kutumiwa vibaya na mkoa mwingine, hivyo Serikali ikaunda taasisi ya mabonde ili kuona rasilimali ya maji inatunzwa vizuri na kuwa kwenye uangalizi wa uhakika.
“Nchi yetu nikimaanisha Tanzania Bara, ina mifumo kumi ya maji (Mifumo miwili ikiunganishwa Wami na Ruvu). Kwa sisi Kanda ya Kaskazini, chanzo chetu kikuu cha maji yote yanayotiririka baada ya mvua kunyesha kabla ya kwenda baharini ni Mto Pangani, ndiyo unakusanya maji yote kwenda baharini, na ndiyo likaitwa Bonde la Pangani, lakini haimaanishi ni Pangani kama wilaya.
“Bali tunapozungumzia eneo letu la Utawala Bonde la Pangani ni kuanzia Mkoa wa Arusha (wilaya mbili Arumeru na Monduli) sababu kule kuna maji tunakusanya kutoka Mlima Meru ambapo kuna mito kule kama Mto Themi, Mto Ngarenaro, Mto Kikuletwa ambayo yatasafirishwa hadi Nyumba ya Mungu na kuingia Mto Pangani. Lakini pia Bonde la Pangani linabeba Mkoa wote wa Kilimanjaro na Tanga, na eneo la Wilaya ya Simanjiro na Kiteto kwa Mkoa wa Manyara” anasema Mhandisi Segule.
***KAZI ZA BODI YA BONDE LA PANGANI
Mhanndisi Segule anasema kazi za Bodi ya Bonde la Pangani kwenye sheria zimeoanishwa 17, lakini yeye ataziweka kwenye mafungu manne (4), ambapo moja ya kazi hizo ni kufanya tathmini ili kujua kiasi cha maji waliyonayo, ambapo wanapozungumzia vyanzo vya maji wameweka kwenye makundi makubwa mawili, maji juu ya ardhi na chini ya ardhi, hivyo lazima wajue maji yaliyopo kwenye hilo bonde.
Kazi ya pili ni kugawa maji mara baada ya kujua wingi wa maji yaliyopo kwenye bonde, na wao ndiyo wenye mamlaka ya kugawa maji hayo kutoka kwenye vyanzo mbalimbali, na hata RUWASA ama Mamlaka za Maji mijini wanapotaka kuchukua maji hayo, mchakato unaanzia Bodi ya Maji Bonde la Pangani, sababu wao wanaangalia maslahi mpaka nje ya mipaka ya wao kwenye maeneo yao ya kazi.
“Sisi ndiyo wenye mamlaka ya kugawa maji kutoka kwenye vyanzo. Na hii ni kwamba wenzetu RUWASA, wenzetu wa Mamlaka za Maji wanapokwenda kutaka maji kwenye chanzo, utaratibu wao wa kisheria unaanzia kwetu kwa sababu sisi tunaangalia maslahi ya watumia maji nje ya mipaka yao wao wa maeneo ya kazi. Mfano DM (Meneja wa RUWASA Wilaya) yeye atashughulikia eneo lake la wilaya, na labda vyanzo vipo pale kwake, na angetamani atumie maji yote anavyotaka.
“Lakini sisi tunajua yale maji yakitoka Wilaya ya Korogwe, kuna mtu wa Muheza anayasubiria, hayo sasa sio mamlaka ya DM. Sisi tunapoangalia maji au kutoa vibali tunaangalia, TANESCO anahitaji maji kiasi gani au huyu hapa anahitaji kufungua shamba, na anahitaji maji ya kiasi gani kwa ajili ya umwagiliaji. Je, kiasi anachochukua kitamuathiri TANESCO! hiyo ndiyo kazi yetu ya pili” anasema Mhandisi Segule.
Mhandisi Segule anasema hata Mradi wa Maji Same- Mwanga- Korogwe, mchakato wake ulianzia kwao namna ya wao kupata maji. Lakini pia mradi mkubwa wa maji wa miji 28, ambapo Mkoa wa Tanga una miji minne (4) ya Handeni, Korogwe, Muheza na Pangani, ambapo Mamlaka ya Maji Safi Handeni na Korogwe (HTM) ndiyo wahusika, mchakato ulianzia kwao, sababu kupitia Mto Pangani, mradi huo utachukua maji lita milioni 50 kwa siku, hivyo bila tathmini ya kina kufanywa miradi hiyo haiwezi kuwa endelevu.
Anasema kazi ya tatu ni usimamizi na utunzaji wa vyanzo vya maji, na hata kiasi cha fedha wanachowauzia maji Mamlaka za Maji mijini na RUWASA ni kidogo sana ili na wao wanapowauzia wananchi waweze kumudu gharama hizo.
“Tunapotoa vibali vya kuchukua maji, sio kwamba tumekaa ofisini, bali wataalamu wangu wanakwenda kujiridhisha kwa kuangalia vitu vingi ikiwemo wingi wa maji. Na katika vibali hivyo tunawauzia kwa fedha kidogo, japo kuna wengine bado wanalalamika wakisema ni bei kubwa. Mfano Tanga- UWASA tunawauzia lita 1,000 kwa sh. 4.50” anasema Mhandisi Segule.
Jambo la nne ni suala la kutatua migogoro inayotokana na watumia maji, na kwa kutumia Jumuiya za Watumia Maji kwenye maeneo yao ya vijiji na kata, wameweza kutatua changamoto hizo ili jamii iweze kuishi kwa amani na kuona shughuli za kiuchumi ikiwemo vyanzo vya maji, mito na visima kunakuwa na uangalizi wa kutosha kwa ajili ya jamii husika.
Anasema wana Jumuiya za Watumia Maji 24 kwenye vidakio tisa (mito midogo inayoingiza maji Mto Pangani) kama vile Mto Kikuletwa (Arusha), Mto Soni (Lushoto), Mto Kerenge (Korogwe), na Mto Umba (Lushoto). Na kuongeza kuwa wakipata nguvu ya kifedha, kila kidakio cha maji wataweka ofisi.
Mhandisi Segule anasema na wao pia wanadhibiti matumizi ya maji kutoka kwa watu binafsi iwe kutaka kuchukua maji kwenye mto ama kuchimba kisima. Ni lazima wajue uwepo wa maji eneo husika, lakini pia wajiridhishe muhusika ni yule aliyeomba huduma hiyo.
Na hata visima vilivyochimbwa Msomera wilayani Handeni, ambapo wananchi wenye asili ya kifugaji kutoka Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCA) ambao wanakwenda huko kwa hiari, vimetafitiwa na watalaamu kutoka Bodi ya Maji Bonde la Pangani.
***VISIMA KWENYE MAJIMBO
Mhandisi Segule anasema kazi waliyotumwa ya kutafiti upatikanaji wa maji kwenye majimbo yote yaliyopo kwenye Bonde la Pangani kuanzia wilaya mbili na majimbo matatu ya Mkoa wa Arusha, Kilimanjaro na Tanga wameshafanya utafiti ambao utasaidia kujua wapi kuna maji ili vyombo vingine kama RUWASA viende vikafanye kazi ya kuwawekea wananchi miundombinu ya miradi ya maji.
MWISHO.
More Stories
Boost ilivyoboresha miundombinu ya elimu Ilemela Judith FerdinandÂ
Samia apongeza walimu 5,000 kupatiwa mitungi ya gesi, majiko kutoka Oryx
Uwekezaji kwenye kilimo utatimiza ndoto ya Samia ya nchi kuwa ghala la chakula Afrika