November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akizungumza na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania –TANESCO (hawapo pichani), Juni 17, 2020 katika Ofisi za Wizara, Dodoma. Kulia ni Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu na kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara, Mhandisi Zena Said.

Bodi ya Tanesco imefanya kazi nzuri – Kalemani

Veronica Simba – Dodoma

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameipongeza Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), akisema imefanya kazi nzuri katika kushughulikia changamoto mbalimbali za umeme nchini.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati), akizungumza na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Juni 17, 2020 katika Ofisi za Wizara, Dodoma.

Alibainisha hayo Juni 17, 2020 alipokutana na kuzungumza na Bodi hiyo jijini Dodoma, akiwa ameambatana na Naibu wake, Subira Mgalu, Katibu Mkuu Mhandisi Zena Said na viongozi wengine waandamizi wa Wizara.

Mojawapo ya kazi zilizotekelezwa na Bodi hiyo, ambazo Waziri anakiri kuridhishwa nazo, ni kushughulikia changamoto ya kukatika-katika kwa umeme katika maeneo mbalimbali nchini, ambayo amesema imetatuliwa kwa asilimia kubwa.

“Changamoto hiyo kwa sasa inatokea mara chache sana, na sababu yake kuu ni matengenezo ya miundombinu ya umeme yanayokuwa yakifanyika katika eneo husika,” alifafanua Waziri na kuitaka Bodi hiyo iendelee kuhakikisha changamoto hiyo inatatuliwa kabisa.

Aidha, Dkt Kalemani aliipongeza Bodi hiyo kwa kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya uzalishaji na usafirishaji wa umeme lakini akaitaka ihakikishe miradi inayoendelea kutekelezwa, inakamilika mapema ili kuwanufaisha wananchi.

Baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na viongozi waandamizi wa Wizara, wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani), alipokutana nao kuzungumzia masuala mbalimbali ya kiutendaji, Juni 17, 2020 katika Ofisi za Wizara, Dodoma.

Vilevile, aliisisitiza kuendelea kusimamia mkakati wa kuiunganishia umeme wa gridi migodi yote ya madini nchini ili kuwawezesha wachimbaji kufanya kazi hiyo kwa tija kwa manufaa yao na ya Taifa.

Katika hatua nyingine, Waziri aliitaka Bodi hiyo kuendelea kubuni mikakati mbalimbali itakayowezesha kuongeza idadi ya wateja wanaounganishiwa umeme kwa mwaka ili kuongeza mapato kwa shirika hilo.

Sambamba na hilo, aliwataka pia kufuatilia na kutafutia ufumbuzi wa kudumu changamoto ya upotevu wa umeme na kuhakikisha umeme wote unaotumika unalipiwa na wahusika.

Baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na viongozi waandamizi wa Wizara, wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani), alipokutana nao kuzungumzia masuala mbalimbali ya kiutendaji, Juni 17, 2020 katika Ofisi za Wizara, Dodoma.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa Bodi hiyo Dkt. Alexander Kyaruzi, alimshukuru Waziri kwa Imani aliyoionesha katika utendaji wao na kumhakikishia kuwa watafanyia kazi maelekezo yote aliyowapa.