April 28, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bodi ya REA yaridhishwa miradi mwambao ziwa nyasa

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOline,Njombe

BODI ya Nishati Vijijini (REB) imeeleza kuridhishwa na kasi na ubora wa utekelezaji wa miradi ya usambazaji umeme katika maeneo ya mwambao wa Ziwa Nyasa yaliyopo katika Wilaya za Ludewa na Makete, ikipongeza juhudi za Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na mkandarasi, Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT).

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ziara ya ukaguzi katika maeneo ya Nkanda na Lumbila, Mjumbe wa Bodi, Florian Haule,amesema Bodi imejionea maendeleo makubwa ya mradi huo unaolenga kusambaza umeme kwa wananchi waishio katika maeneo yenye changamoto za kijiografia wilayani Ludewa na Makete.

Ameeleza kuwa pamoja na ugumu wa miundombinu katika ukanda huo wa Bonde la Ufa, utekelezaji wa mradi unaendelea kwa kasi ya kuridhisha, ambapo kazi ya usimikaji wa nguzo imefikia hatua kubwa na kinachoendelea sasa ni uvutaji wa nyaya.

“Tumefurahishwa na hatua iliyofikiwa. Vifaa vyote muhimu vimeshafikishwa na katika siku chache zijazo tutaanza kushuhudia ufungaji wa transfoma,”amesema Haule.

Kwa mujibu wa Haule, mkandarasi SUMA JKT ameihakikishia Bodi kukamilisha kazi hiyo ifikapo Julai, 2026 ahadi inayotoa matumaini kwa wananchi wenye uhitaji mkubwa wa huduma ya umeme katika maeneo hayo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Mipango na Utafiti REA, Mhandisi Yusuph Ismail, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy, amesema hatua inayofuata ni usimikaji wa transfoma na ujenzi wa njia za umeme za msongo mdogo (LV) ili kuanza kuunganisha wateja wa awali.

Alibainisha  kuwa katika kitongoji cha Nkanda, kazi ya usimikaji wa nguzo kwa umbali wa takribani kilometa tisa imekamilika kwa kiwango kikubwa, huku matarajio yakiwa ni kuwasha umeme ifikapo Mei 25, mwaka huu.
“Tunawahimiza wananchi kufanya maandalizi ya ndani ya nyumba (wiring) ili waweze kuunganishiwa umeme mara moja pindi huduma itakapoanza,” amesisitiza Mhandisi Ismail.

Naye Mkurugenzi Mwendeshaji wa kampuni ya umeme ya SUMA JKT, Meja James Mhame, ambaye pia ni Meneja wa Mradi huo,amesema utekelezaji unaendelea vizuri huku zaidi ya asilimia 80 ya kazi ya awamu ya kwanza ikiwa imekamilika.

“Hatua inayofuata ni uvutaji wa nyaya kwa kiwango kikubwa pamoja na ufungaji wa transfoma ili kuanza kusambaza umeme kwa wananchi wa Nkanda na Lumbila,”amesema Meja Mhame.

Kwa upande wake, Meneja Msimamizi wa Miradi kutoka REA, Mhandisi Deogratius Nagu, alisema Serikali imetenga shilingi bilioni 3.2 kwa ajili ya kutekeleza mradi huo katika Wilaya ya Ludewa, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha vitongoji vyote vinafikiwa na huduma ya umeme.

Amefafanua  kuwa changamoto za kijiografia katika ukanda huo, ikiwemo usafirishaji wa vifaa kwa njia ya maji na kupandishwa milimani, ndizo zilizosababisha REA kulichagua jeshi kutekeleza mradi huo.

“Maelekezo ya Bodi yametutaka kuhakikisha wananchi wote walio tayari wanaunganishwa na umeme kabla mkandarasi hajaondoka. Tumejipanga kuyatekeleza kikamilifu,” alisema Mhandisi Nagu.

Miradi hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kupitia REA za kuhakikisha upatikanaji wa umeme unawafikia wananchi wote wa vijijini, hususan wale wanaoishi katika maeneo ya pembezoni kama ukanda wa Ziwa Nyasa.