September 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bodi ya Mkonge yafafanua malalamiko ya wakulima

Na Hadija Bagsha, Timesmajira Online,Tanga

Mkurungenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania Saddy Kambona,ametolea ufafanuzi masuala mbalimbali yaliyochapishwa kwenye magazeti huku akiahidi kukutana na viongozi wao ili kutatua changamoto hizo zilizojitokeza kwa wakulima wa zao la Mkonge.

Huku amewataka wakulima, viongozi na wananchama wa vyama vya ushirika wa zao hilo kutoleta taharuki kufuatia taarifa mbalimbali zilizochapishwa kwenye baadhi ya magazeti juu ya kinanchoendelea kwenye mashamba na mitambo ya kuchakata zao hilo.

Akiongea na wandishi wa habari jijini Tanga Mkurugenzi Kambona, ameeleza kuwa kuanzia Julai 24,2024 kumekuwa na mfululizo wa makala kwenye magazeti mbalimbali kuhusiana na masuala yanayoihusu sekta ndogo ya Mkonge nchini hususani wakulima wadogo wa zao hilo chini ya Vyama vya Ushirika wa Kilimo na Masoko (AMCOS) vya Hale, Magoma, Magunga, Ngombezi na Mwelya vilivyopo Wilaya ya Korogwe Mkoa wa Tanga.

Saddy amefafanua kuwa mambo yaliyo yaliyoguswa na waandishi wa habari hizo ni Kampuni ya Sisalana kupandisha bei ya huduma ya uchakataji kutoka sh milioni 1 kwa tani hadi sh milioni 1.25 kwa tani, uchakavu wa mitambo ya uchakataji wa Mkonge inayomilikiwa na Sisalana (T) Ltd unaosababisha hasara kwa wakulima.

“Ufafanuzi wa Bodi ya Mkonge ambao ni msimamizi wa sekta ndogo ya zao hilo, hoja hii ni ya kweli, Julai 14,2024 tulipokea barua kutoka Sisalana kuhusu kufanya maboresho ikiwemo hili la kupandisha bei, TSB ilisubiri jibu la AMCOS kuhusiana na hoja za kanuni ya Sisalana,”ameeleza na kuongeza kuwa

“Lakini julai 15 AMCOS waliandika barua kuomba TSB miongozo ya bei ya usindikaji baada ya kupokea hati za madai ya malipo zenye bei mpya ya usindikaji, TSB ilielekeza uongozi wa AMCOS kutolipa ankara hizo mpaka pale suala hilo lipatiwe ufumbuzi na kuamuliwa kwa pamoja baina ya Bodi na Sisalana,”.

Kwa upande wa uchakavu wa majengo, Kambona amekiri kuwa ni chakavu kwa kuwa ni ya zamani tangu enzi za mkoloni lakini ni bora na yenye ufanisi mzuri katika kuzalisha singa bora kuliko sehemu kubwa ya mitambo ya kisasa.

Amefafanua kwamba kampuni zote kubwa za Mkonge kama Amboni Plantation Ltd, Mohamed Enterprises Ltd, Highland Estates yanatumia makotona sawa na Sisalana lakini tofauti ni matunzo, usimamizi na uendeshaji wake.

“Mitambo ya Sisalana ikifanyiwa matengenezo vizuri kama inavyofanyika kwa kampuni za wakulima na kuweka katika ulingano sawa ina uwezo wa kufanya vizuri zaidi na kupunguza hasara ya kutupa singa za wakulima shimoni,”.

Hivyo amwtoa wito kwa kampuni hiyo kufanya matengenezo ya haraka ya mitambo yake hasa katika mashamba ya Magoma, Mwelya na Ngombezi, kwa maana hali ya mitambo ya mashamba ya Hale na Magunga ina nafuu.

Aidha amesema suala la ununuzi wa Mkonge na matatizo yake ni tangu mwaka 2021 kampuni ya Mohamed Enterprises Ltd (MeTL) ilinunua Mkonge kwa miaka mitatu mfululizo na mkataba uliisha Agosti 2023 na haikuongeza mkataba ndio TSB ilipoitisha zabuni ya ununuzi.

Amebainisha kwamba kampuni ya WEFARMTZ ilishinda zabuni kwa bei ya milioni 3.9 na kuanza kununua Mkonge wa AMCOS hadi Aprili 22, 2024 ambapo mkataba ulivunjika kutokana na ukiukwaji wa vipengele vya mkataba.

Amesema baada ya kuvunjika kwa mkataba huo, mshindi wa pili kampuni ya Agriculture Fibers ilisaini mkataba Aprili 22 ,2024 kwa bei ya mshindi wa kwaza na ndiyo inayoendelea mpaka sasa.

“TSB kwa kushirikiana na AMCOS pamoja na Wizara ya Kilimo tumepambana kuletea maslahi ya Mkulima mdogo kwa kulinda bei ya Mkonge isiporomoke, serikali inatumia nguvu nyingi kukuza kilimo hiki, bei nzuri ya Mkonge ni kivutio muhimu,”.

Ambapo ameeleza kuwa hawawezi kuruhusu jitihada za serikali za kuongeza uzalishaji wa Mkonge kufikia tani 120,000 ifikapo 2025/26 zikwamishwe kwa kuweka mazingira ya kuwakatisha tamaa wakulima ya kuendeleza kilimo hichi kwani ni biashara na watahakikisha mkulima mdogo ananufaika.

Vilevile amesema kuhusu suala la umiliki wa makotona baina ya NSSF na AMCOS kwa uwiano wa asilimia 60 kwa 40 mtawalia, lilianza kufanyiwa kazi tangu 2022 ambapo TSB, AMCOS pamoja na Sisalana zilikutana na Msajili wa hazina na kujadili.