January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bodi ya Mfuko wa Barabara yaridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa daraja la JPM

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Bodi ya Mfuko wa Barabara,imeridhishwa na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa daraja la JPM ambao umefikia asilimia 48 huku wakihakikishiwa kuwa ifikapo Februari 2024 litakabidhiwa kwa serikali.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Joseph Haule,wakati wajumbe wa kamati hiyo walipo fanya ziara ya kukagua na kujionea namna utekelezaji wa ujezi wa daraja hiyo unavyoendelea.

“Licha ya changamoto zilizojitokeza za Uviko-19,maji kuongezeka pamoja na miamba kuonekana lakini tumehakikishiwa kuwa ifikapo mwaka 2024 daraja hili litakabidhiwa kwa serikali,”ameeleza Haule.

Haule ameeleza kuwa wamefanya ziara hiyo kwa sababu daraja likishajengwa bodi ndio itakuwa na dhamana ya kuhakikisha linatunzwa kwa umri wake wote ambao limekadiriwa hivyo walitaka kufahamu teknolojia ambayo imetumika,ujenzi jinsi ulivyo endelea ili kujiridhisha ili waje kukabidhiwa kitu kilicho kamilika na kudumu,

“Lengo katika miradi hii ni kuchochea uchumi wa nchi na watu wa eneo husika ,hivyo tumehakikishiwa kuwa vitendea kazi kwa asilimia kubwa vimetoka hapa nchini pamoja na nondo na saruji(cement),kwa maana ya muda wa kukamilika na kiasi cha pesa kitakachotumika tumeambiwa hakutakuwa na ongezeko kwa staili hiyo tumeona nchi itapata kile inachotegemea,”.

Mhandisi Mshauri wa mradi wa ujenzi wa daraja la JPM,Abdulkarim Majuto, ameeleza kuwa mradi huo umefikia asilimia 48.97, ambapo ujenzi unaendelea na mpaka sasa jumla ya nguzo 22 zimeisha jengwa na wameisha laza bimu 13 na watakuwa wanalaza spani baada ya spani mpaka zitimie zote 64.

“Kasi(speed), ya mradi kwa kweli ni nzuri na ina ridhisha kwa maana Mkandarasi anavifaa vya kutosha, material (malighafi) yakutosha, wataalamu wapo lakini kama tunavyoona tuna nguzo jumla 67 sasa hivi nguzo 22,tunatarajia ifikapo Februari 24,2024 mradi utakuwa umekamilika,”ameeleza Majuto.

Kwa upande wake Meneja Msaidizi Ufundi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Mhandisi Rashid Kalimbaga,ameeleza kuwa kazi ya bodi ni kukusanya fedha kwa ajili ya matengenezo ya barabara pamoja na madaraja yake ili kuhakikisha yanakuwa katika ubora wake na yanatumika kwa muda uliopangwa.

“Kwa daraja hili tunawajibu wa kuhakikisha tunapata fedha ili likisha kamilika liweze kupata huduma yote ambayo inatakiwa ya matengenezo na kuhakikisha tunalitunza na linafanya kazi ile iliokusudiwa katika kipindi chote cha miaka 100,bodi imekuja kujiridhisha kama taratibu zote za viwango vimefuatwa,”ameeleza Mhandisi Kalimbaga.

Naye Meneja wa Tanroads Mkoa wa Mwanza Mhandisi Pascal Ambrose, ameeleza kuwa wanatimu yao ya wahandisi kwa ajili ya usimamizi pamoja na Mhandisi Mshauri ambaye ni jicho la serikali katika kuhakikisha kazi inaenda kama ilivyo pangwa.

“Sisi Watanzania bado tunauelewa mdogo wa utunzaji wa mali za serikali,wengi hatuelewi kwamba ni mali zetu wenyewe mtu anadiriki kuiba kitu kwa lengo la kupata mkate wa siku hiyo lakini madhara yanayotokea ni makubwa ya kurudisha maendeleo yetu nyuma na kupiga ‘makertime’pale pale badala ya kusonga mbele na kufanya jambo jingine tunarudia kufanya kile ambacho tumekifanya muda uliopita kulingana na wizi unaoendelea tujifunze kutunza mali za serikali,”ameeleza Mhandisi Ambrose.

Mhandisi Mshauri wa mradi wa ujenzi wa daraja la JPM,Abdulkarim Majuto wa kwanza kushoto akitoa maelezo namna mradi huo unavyoendelea mbele ya wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara walipofanya ziara ya katika daraja hilo ambalo linatarajiwa kukamilika mwaka 2024.(Picha na Judith Ferdinand)
Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Joseph Haule,akizungumza wakati wajumbe wa bodi hiyo walipofanya ziara ya katika daraja hilo ambalo linatarajiwa kukamilika mwaka 2024.(Picha na Judith Ferdinand)
Meneja wa Tanroads Mkoa wa Mwanza Mhandisi Pascal Ambrose ,akizungumza wakati wajumbe wa bodi hiyo walipofanya ziara ya katika daraja hilo ambalo linatarajiwa kukamilika mwaka 2024.(Picha na Judith Ferdinand)
Baadhi ya mafundi wa mradi wa ujenzi wa daraja la JPM wakiendelea na kazi wakati Bodi ya Mfuko wa Barabara iliofanywa ziara ya kutembelea katika eneo hilo.(Picha na Judith Ferdinand)
Meneja Msaidizi Ufundi bwa Bodi ya Mfuko wa Barabara Mhandisi Rashid Kalimbaga ,akizungumza wakati wajumbe wa bodi hiyo walipofanya ziara ya katika daraja hilo ambalo linatarajiwa kukamilika mwaka 2024.(Picha na Judith Ferdinand)
Muonekano wa moja ya nguzo zilizikamilika katika mradi wa ujenzi wa daraja la JPM.(picha na Judith Ferdinand)