Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Bodi ya Mfuko wa Barabara nchini imeitaka Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kuweka nguvu katika ujenzi wa barabara za mawe ambazo zinadumu muda mrefu hivyo kuokoa gharama za matengenezo.
Hayo yamebainishwa na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara nchini, Octavian Mshiu wakati wajumbe wa bodi hiyo walipotembelea na kukagua barabara ya shule ya msingi Igoma yenye urefu wa mita 370 inayojengwa kwa mawe ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 70 na barabara ya Nyashana ambayo tayari imeshakamilika.
Octavian ameeleza kuwa,wametoa wito kuwa siyo Mwanza tu kila Mkoa ambao unaweza kujenga barabara na madaraja kwa teknolojia mbadala wafanye hivyo kwani itakuwa imeisaidia serikali kuokoa fedha nyingi.
“Tutajenga barabara nyingi zaidi za mawe kuliko kutegemea lami ambayo tunaagiza nje ya nchi,”ameeleza Octavian.
Meneja TARURA Mkoa wa Mwanza Gudluck Mbanga,ameeleza kuwa ujenzi wa barabara za mawe mkoani Mwanza umeokoa fedha nyingi ambazo serikali imekuwa ikitumia katika kurudia matengenezo katika barabara za gravu pamoja na kutoa ajira kwa wazawa.
“Kwa kifupi inatusaidia sana kwa sababu Jiji la Mwanza lina miinuko na miinuko yenye mawe na kwenye miinuko barabara hizi za gravu zinashindwa kuhimili na magari yanashindwa kupandisha kwa sababu mvua zikinyesha muunganiko wa mawe na gravu unakuwa siyo mzuri,”, ameeleza Mbanga.
Mbanga ameeleza kuwa Jiji la Mwanza kwa maana ya Wilaya ya Nyamagana na Ilemela wana zaidi ya Km 2000 za barabara huku za mawe ni km 16.
“Ni chache sana asilimia kubwa ya barabara zetu ni udongo tunahitaji sana barabara za mawe kwa kiasi kikubwa tulichofanya ni kama tone sawa na asilimia 0.2, tunashukuru bkuoata vyanzo vya fedha kwa kumalizia barabara hizi ambazo nyinginzipo katika hali siyo nzuri,”ameeleza Mbanga.
Kwa upande wake Mhandisi wa barabara Wilaya ya Nyamagana Jane Mdula, ameeleza kuwa utekelezaji wa ujenzi wa barabara za mawe kwa asilimia kubwa inafanywa na watu na siyo mitambo.
Mhandisi Jane ameeleza kuwa gharama za ujenzi wa barabara za mawe ni nafuu kidogo ukilinganisha na nyingine mfano barabara hiyo ambayo Ina urefu wa mita 370 na gharama yake ni milioni 167.
“,Kwaio tunatengeneza ajira kwa watu wanaochonga mawe ya kujenga barabara ambayo yanachongwa kwa mkono pia ujenzi wake ni WA gharama nafuu ukilinganisha na ujenzi wa barabara nyingine,”ameeleza.
Baadhi ya wafanyakazi katika mgodi wa mawe yanayotumika katika ujenzi wa barabara hizo wameshukuru serikali kutekeleza miradi ya barabara za mawe kwani zimewasaidia kuinua uchumi wao.
“Wakati nakuja Mwanza kutokea Musoma nilikuwa na wakati mgumu kwa sababu sikuwa na ramani lakini kupitia shughuli hii ya kuchonga mawe imenisaidia,”ameeleza Irene Musa.
Naye Monica Mawi,ameeleza kuwa kupitia kazi ya kuchonga mawe ameweza kuwapeleka watoto shule pamoja na kurekebisha nyumba yake.
Hata hivyo Ibrahim Musa,ameeleza kuwa kupitia shughuli ya uchingaji wa mawe yanayotumika katika ujenzi wa barabara zimemsaidia kujiingizia kipato ambacho husaidia wazazi wake.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best