December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bodi ya Kahawa yajipanga kutoa elimu kwa wakulima

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

BODI ya kahawa Nyanda za Juu Kusini (TCB) imesema kuwa katika maonyesho ya sikukuu ya wakulima nane nane mwaka huu watahakikisha wakulima wanaendelea kujifunza namna bora ya utunzaji wa zao la Kahawa ili zao hilo liweze kuwa tija kwa mkulima.

Kauli hiyo imetolewa leo na Ofisa ubora bodi ya Kahawa Nyanda za Juu Kusini, Florian Ndunguru wakati akizungumza na Timesmajira Online katika viwanja vya John mwakangale jinsi walivyojipanga kutoa elimu kwa wakulima wa kahawa wa katika maonyesho ya sikukuu ya wakulima nane nane ambayo kitaifa yanafanyika mkoani Mbeya.

Ndunguru amesema kuwa maandalizi yote yamekamilika kwa ajili ya wakulima kwenda kujifunza mnyororo mzima wa thamani wa zao la Kahawa, uboreshaji mpaka linavyovunwa.

“Amesema wapo tayari kutoa elimu kwa wakulima na wasio wakulima, na mwaka huu kuna mambo makubwa ya kujifunza kuhusu kilimo cha zao la Kahawa tunaamini wakulima walio wengi watabadilika na kuachana na kilimo cha mazoea” amesema Ofisa ubora bodi ya Kahawa.

Aidha Ndunguru amesema kuwa kwa Tanzania wanalima kahawa za aina mbili ambazo ni arabika na robusta lakini zaidi kwa bodi ya Kahawa wanahakikisha aina hiyo ya kahawa ili iweze kumnufaisha mkulima kupitia kilimo cha kahawa.

Hata hivyo Ndunguru amesema kuwa katika maonyesho ya sikukuu ya wakulima nane nane mwaka huu wakulima watarajie elimu kubwa ambayo italeta manufaa na mabadiliko makubwa kwa wakulima wa zao la Kahawa hususani waliopo Vijijini ambao wameona kilimo cha mazoea ni bora zaidi na kusahau kuwa kilimo cha kisasa ndicho kinamtoa mkulima. Saidiana Ngwisa ni Mkulima wa Kata Utengule amesema kuwa bodi ya Kahawa imekuwa ikiwapatia elimu bora namna bora ya kutunza kahawa yao na jinsi ya utunzaji wa zao hili.

“Wakulima tulio wengi hivi sasa tumekuwa na mabadiliko makubwa sanaaa namna ya kulima kahawa ambayo hivi sasa wengi wetu tumebadilika maana tulizoea kilimo cha zamani na kuwa kilimo kisasa hivi sasa ndicho kinatutoa kwa wakulima tulio wengi tumeelimika”amesema.

Naye Rashid Juma mkulima wa Njerenje amesema wakulima walio wengi wamepata hamasa ya kulima zao hilo kutokana na elimu inayotolewa na watalaam kutoka Bodi ya Kahawa Nyanda za Juu Kusini na maafisa ugani kutoka Halmashauri za wilaya.