Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
BARAZA la Michezo la Taifa (BMT) limevijia juu Vyama vya michezo vya Kitaifa ambavyo hadi sasa havijawasilisha mikakati yao kwa mwaka 2020/2021 licha ya zoezi hilo kutakiwa kukamilika toka mwezi Machi.
Itakumbukwa kuwa, hadi Machi mwaka huu ni vyama 39 ndivyo vilivyokuwa vimewasilisha mikakati yao jambo lililomfanya Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), George Msonde kutoa siku saba zilizomalizika Machi 12 kwa vyama vyote vya michezo nchini viwe vimewasilisha mipango yao na kutofanya hivyo ni kukiuka agizo la Serikali na hatua zingechukuliwa dhidi yao.
Agizo hilo la Msonde lilikuwa ni mwendelezo wa agizo la awali lililotolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi mwanzoni mwa Desemba mwaka jana alipokuwa akifungua na kisha kutoa mada kwenye semina ya Maafisa habari na wasemaji wa Vyama, Mashirikisho na klabu mbalimbali za michezo kuhusu namna ya kusemea na kutangaza masuala ya michezo iliyoandaliwa na Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya Kampasi ya Dar es Salaam.
Katika agizo lake, Dkt. Abbasi alidai kuwa, wamebaini kuwa moja ya sababu inayokwamisha timu za Taifa kufanya vizuri Kimataifa ni pamoja na baadhi ya Vyama na Mashirikisho yanayosimamia timu hizo kuzichukulia kama ni zao binafsi na kushindwa kuzigharamia katika maandalizi zinapokuwa na mashindano ya kimataifa jambo linalopelekea kufanya vibaya.
Sababu hiyo ndiyo iliyomsukuma kutoa agizo hilo ambalo lilifungwa rasmi Desemba 31, ambapo zaidi ya vyama 20 viliwasilisha mikakati yao ambayo ilichambuliwa na Maafisa michezo ambao baada ya kukamilisha kazi, aliiwasilisha Wizarani kwa ajili ya utekelezaji.
Licha ya tarehe hiyo kufungwa lakini waliendelea na zoezi la kupokea mikakati ya Vyama na Mashirikisho ambayo yalichelewa kuwasilisha kwa tarehe iliyopangwa huku Kiongozi huyo akiweka wazi kuwa, wao kama walezi licha ya kuwa iliwekwa tarehe maalum ya mwisho wa kuwasilisha mikakati hiyo lakini waliona ni busara kuendelea kupokea ya wale ambao walichelewa kuwasilisha.
Lakini taarifa iliyotolewa jana na Ofisa Uhusiano wa BMT, Frank Mgunga imeweka wazi kuwa hadi sasa vyama vilivyowasilisha ni vile vile 39 ambavyo ni Chama cha Mpira wa Kikapu kwa Watu wenye Ulemavu (Tanzania wheelchair basketball association) TWABA, Chama cha Gofu Wanawake, Shirikisho la Mieleka ya ridhaa, Chama cha Tiba ya Michezo ya Tanzania (TASMA), Chama cha Mchezo wa Kabaddi (TKSA) na Shirikisho la mchezo wa Tenisi.
Pia kipo Chama cha Netiboli Tanzania, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Fitness Instructors Association of Tanzania, Tanzania Body Building Federation, Tanzania Baseball and Softball Association, Tanzania Pool Association, Chama cha Kriketi, Shirikisho la Riadha (RT), Chama cha Taekwon-du, TBRC, Chama cha Mpira wa Mikono (TAVA), Chama cha michezo ya Jadi (CHAMIJATA), TASCA, Shirikisho la Mpira wa Kikapu (TBF) pamoja na Chama cha Mchezo wa kuogelea.
Vingine ni Chama cha Olimpiki Maalum, Chama cha Michezo kwa Viziwi, Chama cha Judo, Kamati ya Paralimpiki (TPC), Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Tanznaia Sailingi Association (TSAA), Automobile Association of Tanzania, chama cha vishale, pamoja na vingine.
Taarifa hiyo imesema kuwa, mara kadhaa wamekuwa wakivikumbusha vyama hivyo kuwasilisha mikakati na kalenda zao za mwaka kwa lengo la kusaidia Baraza kufahamu matukio yao ya kitaifa na kimataifa lakini vingi havijafanya hivyo.
Lakini sasa kuna baadhi ya vyama ambavyo vimeibuka na kutaka kusaidiwa bila kuwasilisha mipango yao au michezo ambayo haipo kwenye kalenda jambo ambalo linaleta ugumu katika utekelezaji na kuonekana kama BMT haitaki kuwasaidia jambo ambalo si kweli.
“Mara kadhaa tumewakumbusha lakini wengi wameendelea kukaa kimya lakini linapokuja tatizo wamekuwa mstari wa mbele kulaumu. BMT ipo makini kuhakikisha michezo yote nchini inapiga hatua na kufanya vizuri ndani na nje na ndio maana tunaendelea kusisitiza vyama kuzingatia mipango pamoja na ratiba zao,”.
“Matukio ya mwaka kuendana na kalenda na kutasaidia kuondo migogoro hii inayoibuka ya matukio mengine kuwepo nje ya kalenza zao hivyo kwa mara nyingine vyama ambavyo havijaleta mikakati na kalenda zao vifanye hivyo haraka,” amesema Mgunga.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania