January 18, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Afisa Habari wa BMT, Najaha Bakari

BMT yashangaa kasi ndogo utendaji wa Vyama, Mashirikisho ya michezo

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

BARAZA la Michezo la Taifa (BMT) limesema linashangazwa na kasi ndogo ya utendaji wa Vyama na Mashirikisho ya michezo hapa nchini kwani hadi sasa hakuna chama chochote kilichowasilisha ratiba na mikakati ya timu za Taifa kwa mwaka 2021 waliyoagizwa kuwasilisha kabla ya Januari Mosi.

Agizo hilo lilitolewa mwanzoni mwa mwezi huu na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi, alipokuwa akifungua na kisha kutoa mada kwenye semina ya Maafisa habari na wasemaji wa Vyama, Mashirikisho na klabu mbalimbali za michezo kuhusu namna ya kusemea na kutangaza masuala ya michezo iliyoandaliwa na Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya Kampasi ya Dar es Salaam.

Katika agizo lake, Dkt. Abbasi alisema kuwa, wamebaini kuwa moja ya sababu inayokwamisha timu za Taifa kufanya vizuri Kimataifa ni pamoja na baadhi ya Vyama na Mashirikisho yanayosimamia timu hizo kuzichukulia kama ni zao binafsi na kushindwa kuzigharamia katika maandalizi zinapokuwa na mashindano ya kimataifa jambo linalopelekea kufanya vibaya.

Sababu hiyo ndio inayomsukuma kutoa agizo hilo ambalo litafungwa rasmi Desemba 31, ambapo mipango na ratiba zote za timu za Taifa zinatakiwa ziwe zimewasilishwa BMT ambao watazipeleka Serikalini ili kujua mwaka 2021 unakuwaje.

Ofisa Habari wa MBT, Najaha Bakari ameuambia Mtandao huu kuwa, licha ya agizo hilo kutolewa na Katibu Mkuu toka Desemba 7 lakini hadi sasa hakuna chama wala shirikisho lolote ambalo limewasilisha mikakati yao ya timu za Taifa kwa ajili ya msimu ujao.

Amesema, wanatambua kuwa yapo mashirikisho mengi ambayo mwakani timu zao zitawakilisha nchi katika michuano ya kimataifa lakini anashangaa hadi sasa hakuna yeyote aliyefuata agizo

“Katimu mkuu aliweka wazi kuwa alitoa agizo hilo baada ya kubaini moja ya sababu inayokwamisha Timu zetu za Taifa kufanya vizuri Kimataifa ni pamoja na baadhi ya Vyama na Mashirikisho yanayosimamia timu hizo kwa niaba ya wananchi kuzichukulia kama timu zao binafsi na kushindwa kufanya maandalizi bora jambo linalotuangusha kimataifa,”.

“Pia aliweka wazi kuwa Disemba 31 mwaka huu mipango na ratiba zote za Timu za Taifa ziwe zimewasilishwa BMT ambapo tutaziwasilisha Serikalini ili tujue mwaka 2021 tunaanzaje, lakini hadi sasa nasikitika kusema kuwa hatujapotea mkakati wowote, ” amesema Najaha.

Aidha amewataka viongozi wanaohusika ndani ya Vyama na Mashirikisho hayo kutumia simu zilizobaki kufanya hivyo kwani wakumbuke kuwa Awamu hii ni ya kazi tu kwenda kwa vitendo hivyo ni lazima kila mmoja afuate maelekezo yanayotoka.

Itakumbukwa kuwa, wakati akihutubia na kufungua Bunge la 12, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Magufuli alieleza kuwa, Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya Sanaa, Utamaduni pamoja na Michezo ambazo zinakua kwa kasi hivi sasa.

Pia alisema kuwa, wataanza kutenga pesa kidogo kidogo kwa ajili ya kuziandaa timu zetu za Taifa ambazo zitakuwa zikijiandaa kwa ajili ya mashindano mbalimbali ya kimataifa ili kuweza kufa nya vizuri.