Na.Mwandishi Wetu,Timesmajira
KATIBU Mwenezi wa Chama cha ACT Wazalendo Taifa, Salum Bimani, ameitaka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kubeba sehemu ya gharama za mafuta ili kupunguza makali ya bei ya bidhaa hiyo na kuwaondolea wananchi mzigo wa gharama za maisha.
Bimani aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi yake iliyopo Vuga, Mjini Unguja.
Amesema kupanda kwa bei ya mafuta kumekuwa tishio kwa maisha ya wananchi kutokana na athari zake katika shughuli za kiuchumi na gharama za maisha, hivyo Serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka kukabiliana na hali hiyo.
Ameeleza kuwa kwa sasa bei ya petroli imefikia shilingi 4,000 kwa lita, huku dizeli na mafuta ya taa zikiwa zimefikia shilingi 4,100 kwa lita.
“Serikali ina wajibu wa kubeba jukumu hili na kupunguza makali ya bei za mafuta. Wananchi wa nchi hii, Unguja na Pemba, ni wanyonge sana na hawawezi kumudu gharama hizi,” alisema Bimani.
Aidha, amesema itakuwa busara kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kubeba sehemu ya gharama za mafuta ili kupunguza bei na kuwawezesha wananchi kumudu gharama za bidhaa hiyo muhimu katika shughuli zao za kila siku.
Ameongeza kuwa kupanda kwa bei ya mafuta ndani ya wiki moja kumeanza kuathiri bei za bidhaa mbalimbali zinazotumiwa na wananchi kila siku, hali inayoongeza gharama za maisha na kuathiri uwezo wa wananchi kumudu mahitaji yao ya msingi.

More Stories
Waziri Homera ashiriki mapokezi ya Rais Samia Uturuki
DC.Chikoka awataka vijana kutumia fursa
Dkt.Kijaji aitangaza Tanzania kimataifa kupitia Islamic Channel