Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema katika mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali kupitia Wizara huyo ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi katika Halmashauri 25 ambavyo ujenzi wake unaendelea.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Wilayani Ileje mkoani Songwe Waziri Ndalichako amesema lengo ni kupata wataalam wa kutosha kutoka katika vyuo vya ufundi stadi nchini lakini pia kuhakikisha dhamira ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda inaweza kufikiwa .
Amesema, katika kuhakikisha nchi inakuwa na uchumi wa viwanda Serikali inaendelea kuwekeza fedha za kutosha katika ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi vya Wilaya na Mikoa, ambapo mpaka sasa tayari vyuo 11 vya Wilaya vimeshakamilika.
Profesa Ndalichako amesema , pia lengo la SeriÄ·ali la kuwekeza katika mafunzo ya ufundi stadi ni kuhakikisha nchi inakuwa na rasilimaliwatu yenye ujuzi na maarifa itakayoshiriki katika uchumi wa viwanda kwa maendeleo endelevu.
“Katika kuhakikisha hilo linafikiwa, Serikali imeendelea pia kutenga fedha za uhakika kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi vya mikoa pamoja na kununua vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia ili kuviwezesha kutoa wataalamu wenye weledi.” amesema Profesa Ndalichako.
Aidha, Profesa Ndalichako amewataka wazazi na walezi nchini kuhakikisha wanawapeleka vijana waliopo mitaani katika vyuo hivyo ili waweze kupata ujuzi na maarifa itakayowasaidia katika kujiendeleza wenyewe kiuchumi na kushiriki katika kutimizi azma ya Serikali ya kuwa na uchumi wa viwanda.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Mstaafu, Nicodemus Mwangela ameishukuru Serikali kwa kukamilisha chuo cha ufundi Ileje kwani ni chuo cha kwanza cha VETA katika mkoa huo ambacho kinakwenda kuwasaidia vijana.
Amesema, mahitaji ya vyuo hivyo nchini ni makubwa sana katika kipindi hiki kwa sababu ya kuongezeka kwa idadi ya vijana ambao kwa sasa ni zaidi ya asilimia 70 ikilinganishwa na watu wazima hivyo ni muhimu kutizamwa kwa lengo la kuleta maendeleo nchini na pia kuongezeka kwa idadi ya shule za Msingi na Sekondori ambazo zinazalisha vijana wengi wasiokuwa na kazi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ufundi Stadi Dkt. Pancras Bujulu amesema, Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi Ileje kina uwezo wa kuchukua wanafunzi 120 kwa wakati mmoja na kimekamilika baada ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kutoa zaidi shilingi milioni 228 kukamilisha ujenzi huo.
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote