April 3, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bilioni 3 kukamilisha ujenzi shule amali Kata ya Choma

Na Lubango Mleka, Times Majira Online Igunga

MBUNGE wa Jimbo la Manonga Seif Khamis Gulamali amesema kuwa Serikali imetoa kiasi cha bilioni 3,ili kukamilisha shule ya amali ambayo inajengwa Kata ya Choma wilayani Igunga mkoani Tabora.

Ametoa taarifa hiyo wakati anazungumza na wananchi wa Kata ya Choma kwenye hafla ya dua ya kuwaombea ndugu na jamaa waliotangulia mbele za haki.Ambapo amesema awamu ya kwanza Serikali imeisha toa kiasi cha milioni 602,na ujenzi umeanza Machi 2025,chini ya Mkandarasi Bajeso Investment Group of Companies LTD kutoka jijini Mwanza.

Amesema shule itakuwa ya bweni na itakapokamilika itachukua wanafunzi kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita,huku akisisitiza wananchi kuendelea kuitunza miradi yote inayoletwa na Serikali katika maeneo yao.

Kwa upande wake Mhandisi Fredrick Mwita,anayetekeleza mradi huo, amesema ujenzi umeisha anza wa madarasa nane,jengo la TEHAMA, maktaba,maabara na utawala pamoja na vyoo na nyumba ya mtumishi.

” Tumepokea kiasi cha milioni 602, kwa ajili ya ujenzi huo kwa awamu ya kwanza ambayo tunatarajia kuukamilisha ujenzi huu ndani ya miezi sita,”amesema Mhandisi Frederick.

Nao baadhi ya wananchi akiwemo,Albert Nicodemus, amesema mradi huo umekuja kutatua tatizo la wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata elimu.