Na Heri Shaaban, Timesmajira Online,Ilala
Halmashauri ya Jiji la Dar-es- Salaam imetenga kiasi cha bilioni 15 kwa ajili ya kukopesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu huku wananchi wakiombwa kuchangamkia fursa hiyo.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Mtaa wa Kisiwani Kata ya Bonyokwa,ambapo amesema kila mwaka mapato ya halmashauri hiyo yamekuwa yakiongezeka,hali inayoongeza kiasi cha fedha kwa ajili ya kukopesha makundi hayo.
Mpogolo,ametumia fursa hiyo kuwahamasisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kuchangamkia mikopo hiyo ambayo inatokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri.
Pia amewataka watumishi wa halmashauri hiyo kuacha kuweka vikwazo na mazingira ya wananchi wanahitaji mkopo kukosa fedha.Kwani Serikali inatoa fedha hizo kwa ajili ya wananchi kunufaika.
Sanjari na hayo amewataka Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kutumia ofisi zao kutatua changamoto za wananchi na kujenga uhusiano mzuri.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Kisiwani, Sulela Logeko,amewahamasisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kujitokeza na kuomba mikopo hiyo ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Pia amesema,wamejipanga vizuri kutatua kero za wananchi hasa ya ulinzi na usalama kutokana na kuwepo kwa matukio mbalimbali ya watu kuvamiwa hasa nyakati za alfajiri.
.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Bonyokwa, Tumike Malilo,amesema utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM unakwenda vizuri katika mitaa yote ya kata hiyo, na katika bajeti ya mwaka 2025/2026 zimetengwa milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya na milioni 70 kuendeleza ujenzi wa kituo cha polisi.
More Stories
Rais Samia amrudisha January kwa Mama,asema kilichotokea ni kumuonya
Milioni 236 kunufaisha vikundi 17 vya wanawake Minazi Mirefu
Mipango 10 kabambe ya TPA