December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bilioni 1.99 kujenga Bwawa la Maji Msomera

Na Zena Mohamed,Dodoma,Timesmajiraonline,Dodoma.

MKURUGENZI Mkuu wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira
Vijijini(RUWASA),Mhandisi,Clement Kivegalo amesema kuwa RUWASA inatumia shilingi bilioni 1.99 kujenga bwawa la maji katika kijiji cha Msomera ili kuboresha huduma ya maji kwa wananchi pamoja na mifugo yao.

Amesema mpango wa utekelezaji wa ujenzi huo umefikia asilimia 15 ambapo uligawanywa katika awamu mbili awamu ya muda mfupi na awamu ya muda mrefu,ambapo awamu ya muda mfupi imekamilika ikiwa na vituo 12 kuchotea maji vilivyoanza kutoa huduma huku awamu ya pili ikifikia asilimia 70 nakutarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Julai, 2022.

Mhandisi Kivegalo amesema hayo jijini hapa leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utendaji kazi wa RUWASA na malengo yake ambapo amesema pamoja na utekelezaji wa mpango wa bajeti 2021/2022, kuliibuka pia uhitaji wa mradi wa maji kwa wananchi wa Kijiji cha Msomera Wilayani Handeni ambako wananchi kutoka Ngorongoro walihamia kwa hiari hivyo ikawalazimu kuwekeza nguvu kubwa katika kuhakikisha wanapata maji.

“Kukamilika kwa awamu hii kutawezesha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wapatao 17,000 pamoja na mifugo yao na kupelekea idadi ya vituo vya maji kuongezeka kutoka 12 hadi kufikia vituo vya kuchotea maji 30 kwa matumizi ya binadamu na vituo 3 kwajili ya kunyweshea maji mifugo,”amefafanua.

Akizungumzia mpango wa RUWASA amesema hadi kufikia mwishoni mwa mwaka wa fedha 2021/2022 jumla ya miradi 303 ilikuwa imekamilika na kumewezesha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wapatao 1,467,107 kupitia vituo vya kuchotea maji 4,147 vilivyojengwa katika maeneo ya vijiji mbalimbali na huku miradi 873 ilikuwa inaendelea na utekelezaji.

Amesema RUWASA ilipanga kutekeleza jumla ya miradi ya maji 1,527, ambapo kati ya hiyo, miradi 1,176 ilikuwa ni ujenzi wa skimu za usambazaji maji, miradi 351 ilikuwa ni ya utafutaji wa vyanzo vya maji chini ya ardhi na miradi 19 ilikuwa ni ya usanifu na jenzi wa mabwawa, ambayo baadaye hutumika kama vyanzo vya maji.

“Miradi 225 kati ya miradi iliyokuwa inaendela na utekelezaji inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Septemba, 2022 na miradi 648 itaendelea na utekelezaji,”amesema.

Ameeleza kuwa Ruwasa inatekeleza shughuli zake kwa kuongozwa na Mpango Mkakati wa miaka mitano, yaani 2020/2021 hadi 2024/2025 ambapo Mpango mkakati huo unalenga pamoja na mambo mengine, kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi waishio vijijini hadi kufikia kiwango kisichopungua asilimia 85 kwa mwaka 2025.

Sambamba na utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2021/22,Mhandisi Kivegalo ameeleza kuwa Sh.Bil.78.53 ambayo ni fedha ya serikali ikiwa ni nyiongeza katika miradi ya maji kupitia UVIKO– 19 kwa ajili ya kutekeleza miradi 172 ya maji vijijini hadi kufikia mwezi Juni, 2022,ilikamilisha jumla ya miradi 68 kati ya 172 imeanza kutoa huduma ya maji kwa wananchi na miradi iliyobaki inatarajiwa kukamilishwa mwishoni mwa Julai, 2022.

“Kukamilika kwa miradi ya UVIKO-19 kutawezesha jumla ya wananchi 1,036,071 kupata huduma ya maji safi na salama.
“Katika mwaka wa fedha uliopita 2021/2022, RUWASA ilipokea jumla ya Sh. 469.4 bilioni kiasi ambacho ni sawa na asilimia 94 ukilinganisha na kiasi cha Sh. 501.5 kilichoidhinishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji Vijijini.

Hata hivyo ametaja changamoto kubwa zilizokuwepo kabla ya kuundwa kwa RUWASA pamoja na huduma ya maji kutokuwa endelevu.

Ambapo amesema kuwa Katika kuhakikisha skimu za maji zilizojengwa katika maeneo ya vijijini zinaendelea kutoa huduma ya maji kwa viwango vilivyokusudiwa, RUWASA imechukua mwelekeo mpya kwa Kuhakikisha kuwa CBWSOs Zinakuwa na Wataalam na Kuwajengea Uwezo.

Ameeleza kuwa hadi sasa, RUWASA imefanikiwa kuunda CBWSOs 2,509, ambazo zimeajiri wataalamu wapatao 5,296 huku
kati ya hao, Mafundi ni 1,837, Wasaidizi wa Hesabu 1,529 na Wasaidizi wa Ofisi 1,930.

“Kuwepo kwa wataalam hao kumewezesha shughuli za kiufundi kufanywa kwa weledi zaidi ikilinganishwa na hapo awali na hii imesaidia kuongeza uhakika wa huduma,”amesema Mhandisi Kivegalo.

“Katika kuhakisha kuwa gharama za uendeshaji wa miradi zinapungua na huduma inakuwa endelevu, RUWASA inashirikiana na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na REA kubadilisha mifumo ya nishati ya uendeshati wa mitambo ya maji kutoka kwenye mfumo wa dizeli kwenda Mfumo wa Umemejua (solar) na umeme wa TANESCO. Hadi sasa, jumla ya skimu ya 19 kati ya 74 za mikoa miwili ya Singida na Dodoma tayari zimebadilishwa kwa kufungwa umemejua.  Kazi hii itaendelea kwa awamu kwa nchi nzima”ameeleza.