December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bilioni 1.6/- zatengwa
kujenga barabara Mbinga

Na Mwandishi Wetu, TumesMajira,Online Mbiga

KAIMU meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Mhandisi Amos Agastin amesema kwa mwaka wa fedha 2021/2022 wametengewa bajeti ya kiasi cha sh. Bilioni 1.6 kwa ajili ya matengenezo ya barabara za rami na changarawe.

Akizungumza na TimesMajira,Online ofisini kwake mwishoni mwa wiki Kaimu meneja huyo amesema kuwa Halmashauri ya Mbinga mji na Mbinga DC zote zilitengewa miradi nane kila Halmashauri, ambapo miradi hiyo imetekelezwa kupitia fedha za Mfuko wa Barabara za matengenezo ya kawaida, fedha za tozo pamoja na fedha za maendeleo za mfuko wa Jimbo sh. milioni 500 ambazo zimetumika kuweka rami barabara ya Mbuyula-Ikulu kilometa 1.5 na ujenzi wa Daraja na mitaro.

Kaimu meneja wa TARURA Wilaya ya Mbinga Mhandisi Amos Agastin akizungumza na waandishi wa habari Jana ofisini kwake.
Lead

Mhandisi Amos alizitaja changamoto wanazokutana nazo katika majukumu ya kazi zao kuwa ni ufinyu wa bajeti, kwani kwa jigrafia ya Mbinga ina mito mingi mikubwa inahitaji ujenzi wa madaraja makubwa kuliko bajeti wanayopata.

“Kipindi cha msimu huu wa mvua barabara nyingi zinajifunga, lakini pia baadhi ya wananchi kuiba mabango yenye alama za barabarani kwenye Wilaya hiyo limekuwa ni tatizo kubwa,”alisema.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliipongeza Serikali kwa kuwachongea barabara kwa kiwango cha changarawe na zingine zimewekwa rami licha ya kuwepo pembezoni mwa mji tofauti na miaka ya huko nyuma walizoea kuona rami zinawekwa mijini tu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya Ovans Construction, Valens Urio ameiomba Serikali kuwaondolea baadhi ya tozo zinazotolewa kwa upande wa Halmashauri na ofisi za madini ambazo ni kero kwa wakandarasi.