January 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bilioni 1.4 zapokelewa ukarabati majengo,vifaa tiba

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Korogwe

HALMASHAURI ya Mji Korogwe (Korogwe TC) mkoani Tanga imepokea kiasi cha bilioni 1.458 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali ikiwemo milioni 50 za umaliziaji wa zahanati ya Lwengera- Darajani na milioni 28 za ujenzi na ukarabati wa vyoo shule za msingi.

Miradi mingine ni ujenzi na ukarabati wa shule kongwe za msingi milioni 180, ujenzi wa nyumba mpya ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Korogwe milioni 180, nyumba nne (4) za Wakuu wa Idara milioni 320, vifaa tiba kwenye zahanati milioni 100 na vifaa tiba kwenye vituo vya afya milioni 600.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga Tito Mganwa akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo. Kushoto ni Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Francis Komba

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Tito Mganwa kwenye taarifa yake aliyoitoa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe.

“Tunaishukuru serikali kwa kutupatia fedha kiasi cha bilioni 1.458, ili tuweze kutekeleza miradi yetu,fedha hizo ni kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali ikiwemo kwenye sekta ya afya na elimu,” amesema Mganwa.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Korogwe Francis Komba amesema fedha hizo zilikuwa ni ombi maalumu waliloomba kwenye bajeti yao ya mwaka wa fedha 2023/2024 na Rais ametekeleza ombi lao.

Madiwani wa Halmashauri ya Mji Korogwe wakiwa kwenye kikao cha Baraza

“Tunamshukuru Rais Dkt. Samia kwa kutupa fedha hizi sababu ilikuwa ni maombi yetu maalumu kwenye bajeti kwa kupata fedha hizi, tutatekeleza miradi mingi ikiwemo ujenzi na ukarabati wa shule,umaliziaji wa zahanati na ujenzi wa nyumba za watumishi,” amesema Komba.

Komba amesema ili kuona miradi iliyopo kwenye halmashauri hiyo inatekelezwa kwa wakati,ubora na thamani ya fedha, Kamati ya Fedha itatembelea miradi kila mwezi bila hata kulipwa posho, ili kujiridhisha ujenzi wake.

Pia Madiwani wa Halmashauri hiyo, watatembelea miradi ya maji, umwagiliaji na barabara ili kujifunza na kuona kazi zinazofanywa na taasisi hizo huku nia ni kuona ubora wa kazi.

Wakuu wa Idara na Vitengo wakiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani Halmashauri ya Mji Korongwe

Komba amesema, ili kwenda na wakati baada ya mabasi kuanza kutembea saa 24, wameamua kufanya ukarabati ikiwemo taa kwenye Stendi Kuu ya Mabasi ya Balozi John Kijazi ya Mjini Korogwe ili yaweze kuingia stendi usiku.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga Francis Komba akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo. Wengine ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Nassoro Mohamed (kushoto) na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Korogwe Tito Mganwa (kulia)