Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Mara
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Jumanne Sagini amefanya ziara ya kutembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara katika eneo la Manispaa ya Musoma wenye thamani ya bilioni 1.4.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo Sagini amesema kuwa, ukikamilika utaipa heshima na hadhi ofisi ya Kamanda wa Polisi kwani kila Kitengo kitakuwa na ofisi yake tofauti na ilivyo kuwa sasa.
“Serikali ni sikivu na nimearifiwa kuwa, fedha za awamu ya pili na tatu tayari zimetoka hivyo basi nimuombe mkandarasi kukamilisha ujenzi kama inavyoelekeza ili ofisi ianze kutumika,” amesema.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara ACP.Salim Morcase, amemshukuru Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Wizara kwa ufuatiliaji wa karibu wa mradi wa ujenzi
“Sisi kama Jeshi la Polisi kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchi tunatoa shukurani zetu za dhati kwa Serikali, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kwako kwa ufuatiliaji wa karibu wa mradi wa ujenzi wa jengo letu,”amesema ACP. Morcase.
Aidha, amebainisha kuwa, utekelezaji wa mradi huo mpaka sasa umefikia asilimia 92 na ulianza kutekelezwa Novemba 18, 2021 unakadiriwa kumalizika mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka 2023.
Muonekano wa Jengo la Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara linalojengwa katika eneo la Manispaa ya Musoma lenye thamani ya bilioni 1.4.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba