November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bil 8/- za Saia zamaliza kero ya maji Buhigwe

Na Allan Vicent, Timesmajira,Online Buhigwe

SERIKALI ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imepeleka zaidi ya sh bil 8/- ili kutekelezwa mradi wa maji katika kata 4 zenye kero kubwa ya maji Wilayani Buhigwe Mkoani Kigoma.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini Wilayani, Mhandisi Francis Molel katika mahojiano maalumu na gazeti hili.

Ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia kwa juhudi kubwa zinazofanyika ili kuhakikisha kero ya maji katika vijiji na kata zote zilizoko katika halmashauri ya Wilaya hiyo zinatatuliwa ili kumtua ndoo kichwani mama.

Amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2022/2023 Rais alielekeza Wizara ya Maji kupeleka zaidi ya sh bil 8/- ili kutekelezwa mradi wa maji wa kimkakati katika kata 4 za Kibande, Mkatanga, Mnanila na Kibwigwa.

Mhandisi Molel amebainisha kuwa mradi huo umekamilika kwa asilimia 95, na baadhi ya wakazi wa vijiji nane wameanza kunufaika na huduma ya maji safi na salama ya bomba kwa mara ya kwanza tangu nchi ipate uhuru.

‘Tunamshukuru sana Rais kwa kuwajali wakazi wa Wilaya ya Buhigwe na kutuletea kiasi hicho cha fedha ili kumaliza kilio cha wananchi, katika hili Mama hana deni, sasa wanaimba mitano tena,’ ameeleza.

Ametaja vijiji vitakavyofikishiwa na huduma hiyo kuwa ni Usagara, Kitambuka, Mkatanga, Nyakimwe, Bweranka, Kibwigwa, Mnanila na Kibande na kuongeza kuwa kati ya Vijiji 44 vya Wilaya hiyo, vijiji 3 tu ndivyo havina mradi wa maji.

Amewahakikishia wakazi wa vijiji hivyo vilivyobakia ambavyo ni Nyaruboza, Rusaba na Nyamiyaga kuwa tayari bajeti imetengwa kwa ajili ya kuwapelekaea mradi wa maji katika mwaka huu wa fedha.

Aidha Mhandisi Molel ameeleza kuwa mradi mwingine wa kimkakati wa sh bil 1.6 tayari umetekelezwa katika Vijiji 4 vya Mlera, Buhigwe, Kavomo na Bwega (Makao Makuu wa Wilaya) na umekamilika kwa asilimia 100.

Ameongeza kuwa mradi mwingine wenye thamani ya zaidi ya sh. mil 900 (Mradi wa Mto Kajana) tayari umetekelezwa katika Vijiji vya Migongo na Kilelema katika kata ya Kilelema na wakazi zaidi ya 200 sasa wameanza kupata maji safi.

Mwisho——————-