Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
WIZARA ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi imepokea shilingi bilioni 64.5 kwa ajili ya kutekeleza Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK) katika Halmashauri 131 nchini ikiwemo shilingi bilioni 50 zilizokopeshwa kwenye Halmashauri 57 kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Ardhi (Plot Development Revolving Fund (PDRF).Â
Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Mei 23,2025 na Waziri wa Wizara hiyo Deogratius Ndejembi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita ambapo amesema fedha hizo zimewezesha upangaji na upimaji wa viwanja 556,191.
Vilevile Ndejembi amesema Wizara hiyo imeandaa programu maalum ya uendelezaji upya maeneo yaliyochakaa katika miji mbalimbali nchini.
“Programu hii itasaidia kuboresha huduma za msingi katika maeneo hayo na hivyo kuyawezesha kuchangia ipasavyo katika Pato la Taifa.
“Programu hii imelenga kuboresha maisha ya wakazi, kupunguza umaskini, kuongeza fursa za kiuchumi na kuhakikisha miji inakuwa endelevu na inayoweza kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kuwa na majengo, miundombinu na huduma bora zaidi kwa Watanzania,”amesema.
Aidha amesema kuw kupitia Programu hiyo, jumla ya maeneo 111 yenye ukubwa wa hekta 24,309.349 yameainishwa katika mikoa 24 kwa ajili ya kupangwa na kuendelezwa upya ili kuwa na tija kiuchumi na kijamii.
“Kwa sasa wizara ina mpango wa kuboresha maeneo chakavu ya Makangira kata ya Msasani, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni,Maanga Halmashauri ya Jiji la Mbeya,Unga Limited Halmashauri ya Jiji la Arusha na Igogo Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
“Hivyo,nitoe wito kwa wadau wote kushiriki kikamilifu katika kufanikisha utekelezaji wa programu hii ili kuleta mapinduzi yatakayobadilisha mandhari na taswira za miji yetu,”amesema Ndejembi.
Pia amesema Wizara imetekeleza Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP).
“Mradi huu umewezesha uhakiki wa mipaka ya vijiji 871 na uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 846 katika halmashauri 21.Aidha, jumla ya vipande vya ardhi 583,734 vimehakikiwa na vimepandishwa katika mfumo wa e-Ardhi,”amesema
Hata hivyo Ndejembi amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeanzisha Kitengo cha Milki ili kuweza kusimamia kikamilifu Sekta ya Milki.
Amesema Serikali imeweza kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wadau mbalimbali wa sekta ya milki na kutoa elimu kwa umma kupitia mikutano mbalimbali na kuratibu uanzishwaji wa vyama vya mawakala katika mikoa mbalimbali.
“Serikali ipo kwenye mchakato wa kutunga sheria ya Milki ambayo itaanzisha mamlaka ya usimamizi wa sekta ya milki (Real Estate Regulatory Authority) ambayo pamoja na mambo mengine itakuwa na jukumu la kuunda mfumo madhubuti wa usimamizi wa sekta ya milki, kutoa taarifa sahihi za wadau na soko la milki na kuongeza ufanisi wa wataalam wa sekta,”amesema.

More Stories
Dkt.Jingu ahimiza matumizi ya TEHAMA katika malezi
LATCU Katavi yasaidia mahitaji ya Mil.5.7 kituo cha watoto yatima,mahabusu
TMA yatoa utabiri wa hali ya hewa wa saa 24 zijazo