Na.Mwandishi wetu, Timesmajira
Serikali imetoa kiasi cha Tsh. Billioni 3.9 kwa ajili ya kuimarisha miundombinu katika Hifadhi ya Taifa Ibanda – Kyerwa iliyoko mkoani, Kagera.
Akikagua miradi ya ujenzi wa miundombinu hiyo Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Musa Juma Kuji amesema Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imetupa upendeleo wa kutupatia fedha za kujenga lango la kuingilia watalii (Complex gate), pamoja na Nyumba za kisasa za Watumishi eneo la Kifurusa hii yote kuhakikisha tunapata mazingira mazuri ya kufanyia kazi zetu.
“Hili ni deni ambalo Rais wetu ametupa sisi TANAPA na hususani watumishi wa Hifadhi hii na tutamlipa kwa kuchapa kazi na kujituma zaidi katika kulinda na kutunza Rasilimali hizi kwa faida ya kizazi cha sasa na kile cha baadae” amesema Kamishna Kuji.
Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Fredrick Mofulu, ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ibanda – Kyerwa, alisema ujenzi wa lango hilo la Hifadhi unahusisha sehemu ya ukaguzi wa nyaraka na malipo, ofisi za wahasibu, ofisi za askari upande wa kuingia na kutokea, ofisi ya Afisa Utalii na msaidizi wake, ofisi ya Tehama, ujenzi wa barabara kilometa mbili, na mifumo ya umeme.
Pia, ujenzi wa vyoo upande wa kuingia, na kutokea vyenye mashimo 7 ya kawaida 1 walemavu kwa kila jengo, uchimbaji wa visima viwili, fensi ya umeme mita 400, Nyumba 2 za watumishi (Jengo 1 kwa familia 2), Nyumba 3 za watumishi (Jengo 1 kwa familia 4), vimbweta 08, sehemu ya kupaki magari makubwa na madogo upande wa kutoka na kuingia lenye ukubwa wa kilometa za mraba 5400, mfumo wa umeme jua, pamoja na eneo la kupumzikia wageni. Kazi ambayo inatekelezwa na Kampuni ya MJT Crew Co. Ltd na JV Sumry’s Enterprises Ltd za hapa nchini ambapo mpaka sasa ujenzi uko asilimia 55 na inatarajiwa kukamilika mwezi Novemba mwaka huu.
Msimamizi wa Mradi kutoka kampuni ya MJT Crew Co. Mhandisi Issa Mfaume ameshukuru menejimenti ya Shirika kwa kuwapatia malipo ya mradi kwa wakati na kupelekea kazi kufanyika kwa ubora unaotakiwa na kuahidi kukamilisha kazi hiyo kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vilivyopo kwenye mkataba wa kazi.
Vilevile, Kamishna Kuji alizungumza na Maafisa na Askari wa Jeshi la Uhifadhi wa Hifadhi ya Taifa Ibanda – Kyerwa na Hifadhi ya Rumanyika – Karagwe na kusitiza utendaji kazi imara ili kusukuma mbele gurudumu la Uhifadhi na Utalii ambalo tumekabidhiwa na Serikali.
“Wapiganaji ndio nguzo ya kupeleka mbele Shirika letu nitoe pongezi zangu za dhati kwa askari wetu ambao jua ni lao na mvua ni yao kuhakikisha Rasilimali hizi zinalindwa na kuwa urithi kwa vizazi vilivyopo na vijavyo” amesema Kamishna Kuji
Aidha, Kamishna Kuji amesisitiza kuwa kila mtumishi ana haki ya kujiendeleza kielimu, haki ya kulipwa posho kwa kila kazi aliyoifanya, haki ya matibabu, likizo, haki ya kupandishwa cheo pale unapotimiza vigezo vyote vya kiutumishi pamoja na haki ya kuthaminiwa kutokana na kazi unayofanya.
Wapiganaji kwa namna mbalimbali wamepongeza jitihada zinazofanywa taasisi katika kutatua changamoto zao na kupongeza namna viongozi wanawafikia katika maeneo yao, wanasikiliza na kutatua changamoto hizo.
“Nikupongeze Afande Kamishna Kuji licha ya majukumu uliyonayo unatoka na kuja kuzungumza na askari, tumekuona Serengeti, tumekuona uko Saanane, sasa Ibanda Kyerwa na Rumanyika Karagwe ukaribu huu kwetu kama askari na kiongozi wa juu wa taasisi unatia hamasa na morali zaidi ya kuchapa kazi“ amesema askari wa uhifadhi daraja la kwanza Henry Joseph Msabila.
More Stories
TAKUKURU,rafiki yanufaisha wananchi Mwanza
Mhandisi Samamba awasisitiza maafisa madini kusimamia usalama wa migoni msimu wa mvua
Wapinzani kutimkia CCM ishara ya ushindi Uchaguzi Serikali za Mitaa