July 1, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bil 1.2 za mapato ya ndani zachochea maendeleo Kaliua

Na Allan Vicent, TimesMajira Onlie, Kaliua

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kaliua, Mkoani Tabora imetumia kiasi cha sh bil 1.2 za mapato ya ndani kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi katika kipindi cha Oktoba-Desemba 2022.

Hayo yamebainishwa juzi na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Jafael Lufungija alipokuwa akiongea na gazeti hili Ofisini kwake ambapo alibainisha dhamira ya halmashauri hiyo kuwa ni kuwaletea maendeleo yanayoonekana wananchi wake.

 Alisema kati ya mwezi Oktoba-Desemba 2022 pekee wametumia kiasi cha sh bil 1.2 za mapato ya ndani kutekeleza miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa nyumba ya Mganga wa zahanati ya Zugimlole na ukamilishaji zahanati ya Limbula.

Miradi mingine ni ujenzi wa Vituo cha afya Ukumbisiganga na Kashishi, ujenzi wa miundombinu ya sekondari za Kazaroho,Mpandamlowoka, Makingi, Konanne na Usenye na ukamilishaji wa miradi ya maendeleo iliyoanzishwa na wananchi.

Aidha kupitia fedha za bakaa ya ruzuku ya miradi halmashauri imetumia kiasi cha mil 395.4 kuendeleza ukamilishaji wa vituo vya afya Igagala. Uyowa na Ilege, zoezi la ukamilishaji zahanati ya Makonge pia linaendelea.

Mwenyekiti alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaongezea kasi ya utekelezaji miradi ambapo wamepokea kiasi cha sh bil 2.1, ambapo sh mil 150 zimetumika kujenga nyumba ya Mkurugenzi na kuboresha miundombinu ya afya.

Aidha sh mil 750 zimetumika kujenga wodi ya wazazi, jengo la upasuaji na jengo la  kufulia katika hospitali ya wilaya na sh mil 100 zimetumika kwenye ujenzi wa zahanati ya Mwendakulima (Uyowa) na ya kijiji cha Ugansa.

Miradi mingine iliyotekelezwa ni ununuzi wa vifaa tiba vya zahanati na vituo vya afya (sh mil 450), ukamilishaji vyumba 8 vya madarasa na matundu ya vyoo katika shule shikizi (sh mil 607.5) na ujenzi wa hosteli Kazaroho Sekondari (sh mil 50).

Akifafanua zaidi Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Jerry Mwaga alisema utekelezaji miradi hiyo umeweza kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi ikiwemo kutoa mikopo nafuu isiyo na riba kwa vikundi vyote vya wajasiriamali.

Alimshukuru Mhesh.Rais kwa kuwaletea kiasi cha sh bil 2.1 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vipya vya madarasa 105 katika shule za sekondari ikiwemo kiasi cha sh mil 250 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya msingi katika kijiji cha Mwongozo.

Aidha alisema wamepokea sh mil 200 kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wasichana na bwalo la chakula katika shule ya sekondari Mwongozo.

Mwaga aliongeza kuwa wamepokea kiasi cha sh mil 156 za Mfuko wa Jimbo kwa ajili ya kuwezesha miradi midogo midogo ya wananchi katika majimbo yote 2 ya Kaliua na Ulyankulu.

Katika programu ya elimu bila malipo alisema wamepokea kiasi cha sh mil 489.7 ambapo sh mil 294.8 ni kwa shule za msingi na sh mil 194.9 kwa sekondari.

Alipongeza Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Kanda ya Magharibi na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) Kanda ya Magharibi kwa kuunga mkono juhudi za serikali katika wilaya hiyo kwa kuboresha sekta ya elimu na afya.

Wakazi wa Wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora wakimiminika kupata huduma bora za afya katika Kituo cha afya Kaliua ambacho ni miongoni mwa Vituo vya afya vilivyoboreshwa na sasa kina miundombinu bora na huduma zinatolewa masaa 24 kila siku. Picha na Allan Vicent.Â